You are currently viewing DAWASA yapeleka tabasamu kundi maalum wiki ya huduma kwa wateja

DAWASA yapeleka tabasamu kundi maalum wiki ya huduma kwa wateja

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira (DAWASA) imehitimisha wiki ya huduma kwa Wateja kwa kutoa misaada kwa wahitaji wenye ulemavu kupitia Shirika lao la Equal Right for All lenye makazi yake Mabibo katika Wilaya ya Ubungo Mkoani Dar es salaam.

Msaada huo umekabidhiwa kwa Asasi ya Haki Sawa kwa Watu Wenye Ulemavu Tanzania na unajumuisha viti mwendo, baiskeli za magurudumu matatu, fimbo za kusaidia watu wenye ulemavu wa kuona, magongo ya kutembelea na mafuta maalumu kwa watu wenye ualbino.

Akizungumza wakati wa kukabidhi vifaa hivyo, Mkurugenzi wa Huduma kwa Wateja DAWASA, CPA (T) Ritamary Lwabulinda, amesema huduma bora kwa mteja haiishii katika upatikanaji wa majisafi na usafi wa mazingira pekee, bali pia inahusisha kujali na kuunga mkono makundi mbalimbali katika jamii.

“Natoa wito kwa jamii kuwashika mkono watu wenye uhitaji ili waweze kushiriki katika shughuli mbalimbali na kuchangia maendeleo ya taifa,” amesema Lwabulinda.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Asasi ya Haki Sawa kwa Watu Wenye Ulemavu Tanzania, Said Halili, ameishukuru DAWASA kwa msaada huo na kuzitaka taasisi na wadau wengine kuiga mfano huo wa kuwajali watu wenye ulemavu.