You are currently viewing Mchuchuma, Liganga kunufaika na mpango wa reli ya Kusini

Mchuchuma, Liganga kunufaika na mpango wa reli ya Kusini

Shirika la Reli Tanzania (TRC) na kampuni ya Arab Contractors ya Misri zimesaini hati ya makubaliano ya kushirikiana katika maandalizi ya mradi wa reli ya Mtwara–Songea–Mbamba Bay, ukiwamo matawi ya Mchuchuma na Liganga, hatua inayoweka msingi wa tafiti za kiufundi na kifedha kabla ya maamuzi ya utekelezaji.

Hafla ya utiaji saini imefanyika Oktoba 16, 2026, jijini Dar es Salaam, ikishuhudiwa na Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa.

Akizungumza baada ya hafla hiyo, Mbarawa amesema Reli ya Kusini ina umuhimu mkubwa katika kufungua fursa za kiuchumi kwa kuunganisha Bandari ya Mtwara na maeneo yanayozalisha mazao ya kilimo, madini na bidhaa za viwandani, hususan miradi ya Mchuchuma na Liganga.

Amesema makubaliano hayo ni hatua ya maandalizi ya mradi, yatakayowezesha kufanyika kwa tafiti za kina kuhusu mahitaji ya usafirishaji, gharama, manufaa ya kiuchumi na njia zinazowezekana za kupata fedha za ujenzi.

Mbarawa ameitaka TRC na Arab Contractors kuandaa mpango wa kazi unaobainisha majukumu ya kila upande, matokeo yanayotarajiwa na muda wa utekelezaji. Pia amesisitiza umuhimu wa tafiti kuzingatia uhalisia wa kiuchumi, mahitaji ya mizigo na uwezekano wa kugharamia ujenzi na uendeshaji wa reli hiyo.

Aidha, amesisitiza kuwa maandalizi ya mradi yanapaswa kuhusisha taasisi muhimu, kujenga uwezo wa wataalamu wa Tanzania na kulinda maslahi ya Taifa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Mhandisi Machibya Shiwa, amesema hati hiyo inaweka msingi wa ushirikiano katika kufanya tafiti na kuandaa mapendekezo ya kitaalamu na kifedha yatakayosaidia kufanya maamuzi kuhusu utekelezaji wa mradi.

Shiwa amesema, kwa mujibu wa makubaliano hayo, Arab Contractors itagharamia tafiti za awali na upembuzi yakinifu. Kampuni hiyo inatarajiwa kuwasilisha taarifa ya awali ndani ya miezi mitatu tangu kusainiwa kwa hati hiyo.

Ameongeza kuwa, baada ya taarifa ya awali kuidhinishwa, kampuni itaandaa upembuzi yakinifu wa kina ndani ya miezi tisa, kisha kuandaa pendekezo la mradi litakalokidhi vigezo vya kupata ufadhili ndani ya kipindi kingine cha miezi tisa.

Kwa mujibu wa Shiwa, TRC itatoa ushirikiano wa kitaalamu, kuratibu taasisi na mamlaka zinazohusika, pamoja na kupitia tafiti na mapendekezo yatakayowasilishwa ili kuhakikisha mradi unakidhi mahitaji ya nchi na unazingatia thamani ya fedha.

Amesema TRC inaendelea kushirikiana na Serikali kupitia Wizara ya Uchukuzi katika kuendeleza sekta ya reli, akieleza matumaini kuwa makubaliano hayo yataisaidia Serikali kufanya maamuzi yenye tija kuhusu mradi unaotarajiwa kuchochea maendeleo ya Ukanda wa Kusini na Taifa kwa ujumla.