You are currently viewing Dkt Samia: Tanzania kufungua tena ubalozi Angola

Dkt Samia: Tanzania kufungua tena ubalozi Angola

Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, amesema Tanzania imeamua kufungua tena ubalozi wake nchini Angola, akieleza hivi karibuni atateua balozi wa kuiwakilisha nchi hiyo, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha uhusiano wa kihistoria na ushirikiano wa kiuchumi kati ya mataifa hayo.

Akizungumza Ikulu jijini Dar es Salaam leo, Oktoba 29, 2026, baada ya mazungumzo na Rais wa Angola, João Lourenço, Dkt Samia amesema nchi hizo zimetiliana saini mikataba minne ya ushirikiano katika sekta za kubadilishana wafungwa, usafiri wa anga, mawasiliano na hali ya hewa.

Katika sekta ya mafuta, Rais Samia amesema Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limeanza jitihada za kushirikiana na Angola.

Amesema pia nchi hizo zimejadiliana kuhusu ushirikiano wa sekta ya madini na masuala ya kikanda, ikiwemo hali ya usalama na amani katika Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Kwa upande wake, Rais Lourenço amezitaka nchi za Afrika kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara badala ya kutegemea zaidi mataifa ya nje.

Amesema Tanzania na Angola zinaweza kunufaika kwa pamoja kupitia rasilimali na fursa zilizopo katika nchi hizo. Ziara yake imefanyika miaka 47 baada ya Rais wa kwanza wa Angola, Agostinho Neto, kuzuru Tanzania mwaka 1979, kufuatia kuanzishwa kwa uhusiano wa kidiplomasia baada ya Angola kupata uhuru mwaka 1975.