Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema miundombinu na mifumo ya teknolojia iliyowekwa katika Mji wa Serikali Mtumba, Dodoma, inapaswa kuongeza tija katika utendaji kazi wa Serikali, kurahisisha utoaji huduma na kupunguza urasimu kwa wananchi.
Akizungumza leo, Oktoba 30, 2026, wakati wa uzinduzi wa Mji wa Serikali Mtumba, Rais Samia amesema wananchi hawapaswi kutumia muda na gharama kubwa kusafiri kutoka mikoa ya mbali kwenda Dodoma kufuatilia huduma ambazo zinaweza kupatikana au kushughulikiwa katika maeneo wanayoishi, akitaja mikoa ya Rukwa, Kigoma na Mtwara.
“Mwananchi kutoka Rukwa, Kigoma, Mtwara asitumie muda na fedha nyingi kuja kufuatilia jambo lake ambalo lingeweza kushughulikiwa alipo,” amesema.
Amesisitiza umuhimu wa kuunganisha mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika taasisi za Serikali ili taarifa zinazopokelewa na kuchakatwa katika taasisi moja ziweze kupatikana na kutumika kwa urahisi katika taasisi nyingine.
Amesema uwekezaji uliofanyika katika Mji wa Serikali Mtumba unapaswa kwenda sambamba na matumizi madhubuti ya teknolojia yatakayorahisisha uratibu wa shughuli za Serikali, kupunguza urasimu na kuhakikisha wananchi wanapata huduma kwa haraka bila kulazimika kufuatafuata ofisi mbalimbali.
