You are currently viewing Rais Samia atambuliwa kimataifa kwa kuhamasisha nishati safi duniani

Rais Samia atambuliwa kimataifa kwa kuhamasisha nishati safi duniani

Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, amepongezwa kwa mchango wake katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, huku akitajwa kuwa mwanamke shupavu anayefanya kazi kubwa katika kuendeleza ajenda hiyo si Tanzania pekee, bali pia Afrika na dunia kwa ujumla.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Ngwaru Maghembe, amesema hayo leo Novemba 13, 2026, katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam, wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya Rais Samia kurejea nchini akitokea Uturuki, alikoshiriki Mkutano wa 31 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP31).

Maghembe amesema Makamu wa Rais wa Uturuki, ambaye alikuwa mwenyeji wa Rais Samia katika mkutano huo, amemsifu Rais kwa juhudi zake katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia na kumtaja kuwa mwanamke shupavu anayefanya kazi kubwa katika eneo hilo.

“Makamu wa Rais wa Uturuki, ambaye ndiye alikuwa mwenyeji wa Rais Samia kwenye mkutano huo, amemsifia sana na kumuita mwanamke shupavu kwa kazi kubwa anayofanya kupambana na nishati safi ya kupikia, si Tanzania tu, bali Barani Afrika na dunia nzima,” amesema Maghembe.

Aidha, amesema Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdoğan, pia amempongeza Rais Samia kwa kazi kubwa anayoifanya katika sekta ya elimu na nishati safi ya kupikia, pamoja na juhudi za kuleta maendeleo kwa Watanzania.

Maghembe amesema katika mkutano huo, Rais Samia alikuwa miongoni mwa viongozi waliopewa heshima ya kushiriki katika ufunguzi wa mkutano huo, ambapo alipata fursa ya kuitangaza Tanzania kwa kueleza fursa zilizopo nchini, ikiwemo upatikanaji wa ardhi kwa ajili ya shughuli za kilimo na uwekezaji unaozingatia uhifadhi wa mazingira.