You are currently viewing TANROADS Mwanza kuwaondoa waliovamia hifadhi ya barabara

TANROADS Mwanza kuwaondoa waliovamia hifadhi ya barabara

Ofisi ya Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) mkoa wa Mwanza imeweka mikakati ya kuwaondoa wananchi waliovamia maeneo ya hifadhi ya barabara na kuendesha shughuli za kibinadamu bila ya kuwa na kibali.

Meneja wa TANROADS mkoa wa Mwanza, Mhandisi Vedastus Maribe amesema kuwa mikakati hiyo ni pamoja na kutoa taarifa ya awali (notice) ya  kuondoka katika maeneo hayo  kwa siku tatu, pia kuweka alama za X zikifuatiwa na maneno ya bomoa au ondoa.

Mhandisi Maribe amesema wataalam wameweka alama hizo kwenye hifadhi za barabara zote za jiji hilo zilizovamiwa na wananchi wanaoendesha biashara mbalimbali ikiwemo ya kujenga vibanda vya mabati pekee na vingine vya matofali.

Amesema kuwa baada ya kukamilika kwa siku walizotangaza TANROADS watalazimika kubomoa vibanda vya biashara,  nyumba na shughuli zote zilizopo maeneo ya  hifadhi ya barabara, na wahusika watatakiwa kulipia gharama za ubomoaji.

Halikadhalika, amesema wananchi wanaotaka kutumia maeneo ya hifadhi ya barabara wanatakiwa kufuata taratibu za kupata kibali kwa mujibu wa sheria namba 13  ya mwaka 2007.

Kwa upande wao wananchi wa maeneo ya Usagara, Nyashishi na Buhongwa ambayo yameathirika kwa sehemu kubwa ya barabara kuathiriwa na wafanyabiashara walioweka bidhaa zao mita chache kutoka kwenye barabara, wamesema wamepokea taarifa za kuondoka maeneo hayo na sasa wanasubiri utekelezaji.