Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
SHIRIKA la Reli Tanzania (TRC) limetangaza kuongeza safari za treni kati ya tarehe 27 Juni, 2025 na 28 Juni, 2025 kutoka Dodoma kwenda Dar es Salaam kwa treni za EMU maarufu Mchongoko.
Ongezeko la safari hizi ni kukidhi mahitaji ya usafiri kwa wananchi na wadau mbalimbali wanaosafiri kutoka Dodoma kurejea katika maeneo yao hususani Jijini Dar es Salaam na miji mingine baada ya kuhitimishwa kwa shughuli za Bunge.
Ratiba ya safari hizo za nyongeza zitakuwa kama ifuatavyo; Juni 27, 2025: Treni itaondoka Dodoma kuelekea Dar es Salaam saa 1:20 usiku na Juni 28, 202S treni itaondoka Dodoma kuelekea Dar es Salaam saa 12:50 asubuhi.
Katika taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Kitengo cha Habari na Uhusiano, Fredy Mwanjala imesema TRC inaendelea kuwahimiza abiria kuzingatia muda wa kufika stesheni wa angalau saa mbili kabla ya safari.
Aidha, linasisitiza abiria kukata tiketi mtandao kupitia tovuti sgrticket.trc.co.tz ama stesheni za Shirika ili kuepuka usumbufu.