Serikali inaendelea kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati ya nishati mkoani Kigoma, inayolenga kuimarisha upatikanaji wa umeme wa uhakika na kuchochea maendeleo ya sekta mbalimbali, ikiwemo uchukuzi kupitia usafiri wa reli, anga, barabara na maji.
Upatikanaji wa umeme wa uhakika utasaidia kuboresha huduma za usafirishaji, kuongeza ufanisi wa shughuli za bandari, viwanja vya ndege na vituo vya reli, pamoja na kuwezesha huduma za karakana, maghala ya mizigo na mifumo ya mawasiliano.
Hatua hiyo itachangia kupunguza gharama za uendeshaji, kurahisisha usafirishaji wa abiria na mizigo na kuvutia uwekezaji katika sekta ya uchukuzi.
Miongoni mwa miradi hiyo ni ujenzi wa kituo cha kuzalisha umeme kwa kutumia maji ya Mto Malagarasi, wilayani Uvinza, chenye uwezo wa kuzalisha megawati 49.5.
Mradi huo ulianza Aprili 30, 2024, na unahusisha pia ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa kilovoti 132 yenye urefu wa kilomita 54 hadi kituo cha kupoza umeme cha Kidahwe. Hadi sasa, mradi umefikia asilimia 31.7 ya utekelezaji.

Mradi mwingine ni ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa kilovoti 400 kutoka Nyakanazi hadi Kigoma yenye urefu wa takribani kilomita 280, pamoja na upanuzi wa kituo cha Nyakanazi na ujenzi wa kituo kipya cha kupoza umeme cha Kidahwe.
Aidha, Kigoma iliunganishwa na gridi ya taifa Desemba 2024, hatua inayolenga kupunguza utegemezi wa mitambo ya dizeli na kuongeza uhakika wa upatikanaji wa nishati kwa shughuli za kiuchumi.
Miradi hii ina thamani ya jumla ya Shilingi bilioni 817.99, ambapo Shilingi bilioni 328 ni kwa Mradi wa Malagarasi na Shilingi bilioni 489.99 ni kwa mradi wa njia ya kusafirisha umeme ya Nyakanazi-Kigoma.
Kukamilika kwa miradi hiyo kutafungua fursa za uwekezaji katika huduma za uchukuzi, kuimarisha usafirishaji kupitia Ziwa Tanganyika, reli, anga na barabara, pamoja na kuongeza ufanisi wa biashara ya ndani na kuvuka mipaka.
Hivyo, uwekezaji katika miundombinu ya umeme unatarajiwa kuwa kichocheo muhimu cha kuifanya Kigoma kuwa kitovu cha usafirishaji na lango la fursa za kiuchumi na biashara katika ukanda wa Magharibi mwa Tanzania na nchi jirani.
