You are currently viewing Tanzania kuratibu mafunzo ya kibingwa kwa wataalamu 60 wa afya Afrika

Tanzania kuratibu mafunzo ya kibingwa kwa wataalamu 60 wa afya Afrika

Tanzania itaratibu nafasi 60 za mafunzo ya kibingwa kwa wataalamu wa afya kutoka nchi mbalimbali za Afrika, katika hatua ya awali ya Mpango Elekezi wa Kuboresha Afya ya Mama na Mtoto Afrika 2026–2030.

Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa, amesema hayo leo Ikulu, Dar es Salaam, akieleza utekelezaji wa maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan yaliyotolewa wakati wa ufunguzi wa CPHIA 2026, Addis Ababa, Ethiopia.

Amesema mafunzo hayo yatalenga maeneo yenye uhitaji mkubwa, yakiwamo ukunga, magonjwa ya wanawake na uzazi, usingizi na ganzi, pamoja na huduma za watoto wachanga, kuongeza wataalamu wenye ujuzi maalumu.

Mchengerwa amesema mpango huo pia utaimarisha huduma jumuishi za afya ya uzazi, mama, watoto na vijana balehe, kwa kuunganisha huduma za wajawazito, uzazi salama, chanjo, lishe na mifumo ya rufaa.

Amesema sekretarieti ya Kinara itashirikiana na Umoja wa Afrika na Africa CDC kufuatilia utekelezaji, kwa kutumia mifumo ya taarifa za afya na Jedwali la Tathmini ya Rais lenye viashiria saba vya msingi.