Afghanistan imeonesha nia ya kuwekeza katika madini ya vito mkoani Tanga, huku ujumbe wa wafanyabiashara wa sekta ya madini kutoka nchini humo ukitarajiwa kutembelea Tanzania mwezi Julai 2027 ili kutathmini fursa za uwekezaji.
Nia hiyo ilielezwa katika kikao kati ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe. Balozi Batilda Burian, na Waziri wa Viwanda na Biashara wa Afghanistan, Mhe. Alhaj Nooruddin Azizi. Kikao hicho kilifanyika kando ya Mkutano wa Kimataifa wa Uwekezaji katika Sekta ya Madini (TMIC 2026), uliofanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Novemba 19 hadi 21, 2026. Pia kilihudhuriwa na Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Tanga, Mhandisi Laurent Bujashi.
Katika kikao hicho, Balozi Burian aliwaeleza wajumbe kuhusu fursa za uwekezaji katika madini ya vito yanayopatikana mkoani Tanga, yakiwemo sapphire, garnet, tourmaline, ruby na spinel. Aliwaalika wafanyabiashara kutoka Afghanistan kuwekeza katika sekta hiyo mkoani humo.
Kwa upande wake, ujumbe wa Serikali ya Afghanistan ulieleza utayari wa kuleta wafanyabiashara wa sekta ya madini nchini Julai 2027 ili kutembelea maeneo yenye madini hayo na kutathmini fursa zilizopo.
Kupitia Investor Deal Room ya TMIC 2026, wadau walipata nafasi ya kufanya mazungumzo ya kibiashara, kujadili fursa za uwekezaji na kuweka msingi wa ushirikiano katika sekta ya madini, ikiwemo kuongeza thamani ya madini ya vito hapa nchini.
