You are currently viewing DC Magu awaasa wananchi kudumisha amani, kuimarisha familia

DC Magu awaasa wananchi kudumisha amani, kuimarisha familia

MKUU wa Wilaya ya Magu, Jubilate Lawuo amewataka wananchi wa wilaya hiyo kuendelea kudumisha amani na utulivu hususani katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29 mwaka huu.

Pia amewasisitiza kuendelea kumuombea Rais Samia Suluhu Hassan ili kulivusha salama Taifa katika kipindi hiki lakini pia kuziombea familia ili zitambue wajibu wao wa kulea watoto na kutokomeza wimbi la watoto wa mitaani.

Lawuo ametoa wito huo leo Alhamisi wakati akiwaongoza viongozi wa dini, kamati ya ulinzi na usalama, watumishi wa serikali na wananchi wa wilaya hiyo waliokusanyika katika uwanja wa Mwanankanda kuombea amani katika uchaguzi mkuu ujao unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29 mwaka huu.

“Nimewaalika ndugu zangu viongozi wa dini kutusaidia maombi maalumu kwa sababu mwaka huu tuna jambo kubwa la uchaguzi hivyo ninawaomba mtusaidie kuombea amani katika wilaya yetu.

“Lakini pia tuwaombee wazazi watambue wajibu wao, wasiwatelekeze watoto kwa sababu katika kipindi cha miaka miwili nilichokuja hapa nimekumbana na wimbi kubwa la watoto wanaozagaa mitaa kutokana na kutokuwa na walezi,” amesema.

Katika dua hiyo, Paroko wa Parokia ya Magu Jimbo kuu la Mwanza, Padre Onesmo Shingelwa ambaye ni Katibu wa jumuiya ya viongozi wa dini wilayani humo, ilijumuisha makundi ya viongozi mbalimbali akiwemo Sheikh wa wilaya ya Magu, Nuhu Zaid Khamis.

Makundi hayo ni pamoja na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Umoja wa Maaskofu wa Makanisa ya Kipentekoste (CPCT), Umoja wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) na Kanisa la Ukombozi.

Leave a Reply