MKURUGENZI Mtendaji wa Halmashauri ya Wikaya ya Magu mkoani Mwanza, Mohamed Ramadhani ametoa wito kwa Watu wanaoishi na Virusi Vya Ukimwi (WAVIU) wilayani humo kutambua kuwa mtaji namba moja kwa binadamu ni afya.
Pia amewataka kuendelea kujali afya zao na kutoa elimu kwa jamii ili itambue kuwa mtu akipata maambukizi ya VVU sio mwisho wa uhai wake bali ni kujitambua na kuendelea kuishi kwa utaratibu kwa sababu UKIMWI hautishi tena.

DED Ramadhani ametoa wito huo mwishoni mwa wiki wakati akikabidhi msaada wa baiskeli 66 kwa WAVIU washauri wilayani Magu pamoja na vifaa saidizi vilivyotolewa na Shirika linaloshugulikia mapambano ya Ukimwi -ICAP kwa kushirikiana na Serikali.
Akikabidhi baiskeli hizo, buti, makoti ya mvua na notebook, Mkurugenzi huyo amewataka WAVIU hao washauri kutumia zana hizo kwa malengo yaliyokusudiwa na matumizi ya kawaida lakini pia kuvitunza.
“Leo tunapewa mguu unaokwenda kukuongezea ufanisi na kukupunguzia muda uliokuwa unautumia kwenda na kurudi kuhudumia jamii
“Pamoja na kwamba utatusaidia kutekeleza majukumu yetu ila utatusaidia mambo ya kimaisha. Nitakapokuta umeshindwa kubadilisha ‘chubu’ nitakushangaa. Kwa sababu ICAP imekurahisishia tu,” amesema.

Awali akimkaribisha mkurugenzi katika hafla hiyo, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Magu, Dk. Mhana Raphael amesema hadi sasa asilimia 97 ya watu waliopimwa na kubainika kuwa na VVU wanatumia dawa za kufubaza makali ya VVU- ARVs.
Pia amesema asilimia 98 kati yao wanatumia kwa uaminifu dawa hizo huku akina mama wajawazito wakiongoza kwa kufuata utaratibu.
Pia amewatoa hofu WAVIU hao kuwa serikali imeweka mikakati imara kuhakikisha dawa hizo zinaendelea kutolewa kwao.
Naye Mratibu wa kudhibiti UKIMWI, homa ya Ini na Magonjwa ya ngono, Dk. Shamila Mkufya amesema msaada huo wa baiskeli umelenga kuwasaidia WAVIU washauri kutembelea watumiaji wa ARVs kwenye jamii kuwaelimisha pamoja na kuwahamasisha namna ya kujitambua na kuishi kwa utaratibu.
Naye Mwenyekiti wa WAVIU Washauri wilayani humo Herman Ngika mbali ya kushukuru kqa msaada huo ameahidi kuwa wataendelea kufanya kazi hizo kwa kujitolea.
WAVIU washauri ni watu wanaoishi na maambukizi ya virusi vya Ukimwi na wamejiweka wazi na huru kuwashauri watu wanaoishi na VVU katika nyanja mbalimbali ikiwemo ufuasi mzuri wa dawa, kutoa ushauri nasaha kwa wenzao, kujitolea kufuatilia na kufundisha kwa njia ya ushuhuda wa maisha sambamba na kuhamasisha Waviu kujiunga katika vikundi ili kusaidiana na kupunguza unyanyapaa.
