Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, amemtaka Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) Camilius Wambura, kuangalia namna jeshi hilo litakavyojenga imani yake kwa wananchi, sekta binafsi na jumuiya za kimataifa zilizopo hapa nchini.
Mkuu huyo wa nchi ametoa kauli hiyo, akirejea utafiti uliochapishwa na Shirika la Afrobarometer hivi karibuni, ukihusisha wananchi wa Afrika na imani kwa Jeshi la Polisi.
Kupitia utafiti huo, wananchi hao walihojiwa endapo watapata shida ya kisheria, imani yao ikoje kwa Jeshi la Polisi na ripoti imeonyesha asilimia 12 pekee ya Watanzania waliohojiwa walisema watakimbilia polisi.
Katika nchi 38 za Afrika zilizohusishwa kwenye utafiti huo, moja pekee ndiyo ilikuwa na alama za juu yaani asilimia 25, kwamba raia wakipata shida watakimbilia polisi.
Rais Samia ametoa maelekezo hayo kwa IGP Wambura, leo Mei 28, 2026 wakati akihitimisha Mafunzo ya Maofisa na Wakaguzi Wasaidizi wa Polisi, Kurasini, Dar es Salaam leo Mei 28, 2026.
Amesema taarifa hizo si za kuzibeza, bali ni kuangalia changamoto zilipo hadi wananchi wajibu hivyo na zifanyiwe kazi.
“Tunataka kuona namna Jeshi la Polisi linavyojenga imani yake kwa wananchi na sekta binafsi na jumuiya za kimataifa zilizopo nchini. Hapa tunaangalia legitimacy (uhalali) ya polisi,” amesema.
