Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan, amewaapisha majaji tisa wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania, akiwataka kwenda kuimarisha utendaji wa haki na kulinda uhuru wa mhimili huo nchini.
Pia, Dkt Samia amewaambia majaji hao, wamepata uteuzi huo kutokana uzoefu, weledi na utumishi utumishi waliounyesha katika nafasi zao mbalimbali walizotumikia Mahakama.
Dkt Samia ameeleza hayo leo Jumanne Mei 26,2026 Ikulu ya Dar es Salaam, wakati wa hafla ya kuwaapisha majaji hao aliowateua hivi karibuni.

“Hii ni ishara ya kuwa mmefanya kazi nzuri na Tume ya Utumishi ya Mahakama imeitambua kazi yenu na imewapendekeza kupandishwa katika ngazi hii,” amesema Dkt Samia na kuongeza kuwa;
“Imani yangu kwamba kwa heshima hii mliyopewa mtafanya kazi kwa bidii zaidi, nendeni mkaongeze nguvu kwenye Mahakama ya Rufani, kwa kutambua umuhimu wa haki kama msingi wa amani, utulivu, maendeleo ya Taifa na ustawi wa wananchi kwa ujumla,” amesema.
Amewataka majaji hao kwenda kuitumikia nchi kwa weledi na uzalendo kama walivyokula kiapo,”mmeapa mtafanya kazi bila upendeleo, huba na chuki. Kuna haka ka huba na kachuki sijui… nataka mkatizame vizuri ndani yenu katika kutoa uamuzi wa hukumu zenu,”
Amewaambia majaji hao kuwa dhamana hiyo si ya cheo tu, bali kulinda haki za Watanzania, na katika maamuzi wanayoyafanya, wakumbuke kuwatumikia wanadamu ni kumtumikia Mungu.
“Nimeshawaambia mara kadhaa, kwa hapa duniani ukiacha Mungu anayesimamia haki za wote, wengine ambao Mungu amewateua kusimamia haki za wenzenu ni nyinyi majaji katika ngazi tofauti. Kwa hiyo mnafanya kazi kubwa, hivyo mnadhima kubwa katika nchi katika kutenda haki,” amesema.
