You are currently viewing Dkt Samia: Sitaki wakuu wa mikoa wachafu

Dkt Samia: Sitaki wakuu wa mikoa wachafu

Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, amewataka wakuu wa mikoa wote nchini kusimamia usafi wa mazingira katika maeneo yao, akieleza kwa sasa baadhi ya maeneo hali si nzuri.

Kwa mujibu wa Samia, kitendo cha kuwapa madiwani zabuni za usafi ndio kinachosababisha uchafu, kwa sababu hawana uwezo wa kusimamia suala hilo, hivyo halmashauri zinapaswa kubadilika na kuwapa wakandarasi wenye uwezo.

Dkt Samia ameeleza hayo Jumatano Septemba 2,2026 wakati wa akiwaapisha wakuu wa mikoa na katibu tawala aliowateua hivi karibuni. Uapisho huo umefanyika Ikulu Ndogo ya Tunguu, Kusini Unguja.

“Kuna watu wanaweza, wanaomba lakini mnawanyima.Mnawapa madiwani ili mkae nao vizuri, hawa uwezo, miji michafu, imeenea uchafu kila pembe aibu, hatuwezi kuendelea hivyo, nendeni mkasimie usafi, asiyeweza aondolewe,” amesema.

Katika uapisho huo, Rais Samia aliutaja Mkoa wa Dar es Salaam (uso wa Tanzania) akisema hajaridhika na suala la usafi, hasa katika mitaa yake, akiahidi kukaa nao kikao na watendaji wao mkoa huo.

“Lazima tuimarishe usafi wa nchi yetu, tuondoe uchafu. Tunapovutia watalii, mtalii hana kikomo, anapenya penya, kuna wengine wataka kuona tu Dar es Salaam ipoje,” amesema Dkt Samia.