You are currently viewing Dkt Samia: Wanaoutaka urais 2030 wasituvurugie nchi

Dkt Samia: Wanaoutaka urais 2030 wasituvurugie nchi

Rais Samia Suluhu Hassan amewataka wenye nia ya kuwania urais mwaka 2030 wasiivuruge nchi, huku akiwasihi wateule wake wenye dhamira hiyo wapishe ili wakafanye harakati hizo wakiwa nje ya Serikali.

Amesema kazi iliyopo sasa ni kutibu majeraha yaliyotokana na vurugu za Oktoba 29, hivyo watu wasitengeneze matarajio ya mwaka 2030 kwa kuwa mpangaji wa yote ni Mungu.

“Nimesema kazi yetu sasa ni kutiba majeraha na hapa nataka nizungumze na watoto wangu ‘vijana’ wanaoangalia mbele hawa wengine waliopo nje. Wanaongalia mbele 2030 safari hiyo isiende kutuvurugia nchi yetu.

“Nilizungumza na mawaziri wangu, nikamwambia namuangalia mmoja mmoja, una maslahi na huko, kaa nje kafanye huko usifanye ndani ya Serikali yangu.Nimekuweka hapo ukatumikie wananchi ‘interest’ yako utaikuta mbele, Mungu ndio anajua nani kiongozi,” amesema.

Amesema mtu anaweza kujipanga na kuwa na mikakati, lakini usifanikiwe, akitolea mfano wapo waliokuwa na uwezo wa kifedha, wakajiandaa kwa mbio za urais, lakini hawakufanikiwa.

Dkt Samia ameeleza hayo leo Jumanne Disemba 2,2025 akizungumza na Wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), Jijini Dar es Salaam.

Leave a Reply