You are currently viewing EACOP kuboresha mazalia ya Sungura, pomboo na ndege wa Burigi

EACOP kuboresha mazalia ya Sungura, pomboo na ndege wa Burigi

IMEELEZWA kuwa Mradi wa bomba la mafuta ghafi wa Afrika Mashariki (EACOP) kupitia programu ya urejeshaji na ulinzi wa viumbe hai wa baharini na ajira katika mwambao wa Tanga, unatarajiwa kuwanufaisha sungura, pomboo na ndege wa Burigi katika kuendeleza mazalia ya viumbe hai hao.

Programu hiyo inayogharamiwa na EACOP inalenga kulinda mazingira kutokana na ujenzi wa temino ya mafuta ghafi katika Ras ya Chongoleani itakayowezesha kusafirisha mafuta katika masoko ya kimataifa.

Hayo yamebainishwa na Mshauri na mwanasayansi wa masuala ya bahari wa EACOP, Metthew Richmond katika mkutano wa siku mbili, uliofanyika hivi karibuni mkoani Tanga na kuwakutanisha wataalamu wa taasisi zinazotekeleza miradi 10 ya kurejesha mazingira ya asili ya mwambao wa Tanga.

Alisema EACOP ina jopo kubwa la wataalamu wanaokidhi vigezo na kwamba wamefanya tafiti na kugundua kuwa wanaweza kustawisha eneo zima la Chongoleani na maeneo yote ya jirani.

Alisema katika kujenga temino Chongoleani, EACOP inawajibika kutekeleza maagizo ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IFC) linaagiza anayetelekeza mradi ahakikishe hakuna madhara kwa wananchi wa eneo husika na ahakikishe pia wananchi wanashiriki katika maamuzi yanayofanywa na mwenye mradi.

Alisema EACOP ilibuni programu ya Mwambao wa Tanga yenye miradi kumi tofauti ili kutekeleza ya matakwa hayo ya IFC, kwani ujenzi wa temino unavuruga mazingira ya bahari katika mwambao  katika eneo la Chongoleani.

“Miongoni mwa viumbe vya bahari ambavyo vipo katika hatari ya kupotea ni pamoja na samaki aina ya pomboo. Hivyo kwa mradi huu wa urejeshwaji wa nyasi utasaidia nao pia kuongezeka kwa viumbe hao,” alisema Richmond.

Aidha, Kiongozi wa nyasibandia, kutoka Shule Kuu ya Sayansi na Teknolojia ya Uvuvi, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Blandina Rugendo, alisema zoezi la kulinda bahari katika mwambao wa Tanga linaendelea vizuri. 

“Sisi ni wadau katika programu hii.  Mradi wetu unaendelea na ni salama kabisa. Nyasi zitavutia samaki wengi kuishi katika eneo hilo na hili litakuwa na jita kwa wavuvi,” alieleza Dk. Rugendo.

Naye Afisa Uvuvi wa Jiji la Tanga, Gladys Manyika alieleza kuridhishwa na utekelezaji wa mradi wa urejeshwaji wa mazingira ya asili ya bahari, na kusema kwamba sasa ni dhahiri kwamba mradi hautaadhiri shughuli za uvuvi bali utakuwa na tija kwa wavuvi.

Alisema kuwa wenyeji wa eneo hilo wengi wao wameajiriwa kwenye mradi kwa kazi mbalimbali za ujuzi wa kati na ujuzi wa chini.

Manyika alitaja maeneo ambayo  wamepanga mradi  upande nyasi bahari ni pamoja na Mabopweni, Mpirani, Putini na Ndaoya.

EACOP inatekeleza kampeni ya Serikali ya Tanzania inayosisitiza upandaji wa miti. Kampeni hiyo ilizinduliwa rasmi Juni 20, 2024.  Lengo la kampeni hiyo ni kuzuia kasi ya upotevu wa miti ili kupambana na kuibuka kwa ukame na ukosefu wa mvua.

Urejeshwaji wa nyasi mwambao wa Tanga ambao utasaidia kuongezeka kwa pomboo, unahusisha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Licha ya EACOP kupanda nyasi katika maeneo ya bahari lakini pia wanalinda wanyama pori  ambao wako katika hatari ya kutoweka kama vile sungura na baadhi ya ndege wanaopatikana katika hifadhi ya taifa ya Burigi Chato. 

Pamoja na kupanda nyasi bahari katika eneo la Chongoleani pia EACOP wametoa miti 12,600 kwa Idara ya misitu ya nchini Uganda kwa ajili ya kuunga mkono juhudi za nchi za kupanda miti 40,000 kwa lengo la utunzaji wa mazingira.

Bomba la EACOP, lenye urefu wa kilometa 1443, linaanzia Wilaya ya Hoima nchini Uganda na kuishia nchini Tanzania katika Mkoa wa Tanga. Bomba hilo limepita katika mikoa nane ya Tanzania bara ambayo ni Kagera, Geita, Shinyanga, Tabora, Singida, Dodoma, Manyara na Tanga.

Leave a Reply