Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) umekabidhi mashine ya kisasa ya uungaji mabomba (Orbital Welding Equipment) kwa Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) Dodoma, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa sera ya kuwawezesha wazawa (Local Content) inayolenga kuwajengea uwezo Watanzania ili wanufaike na utekelezaji wa miradi mikubwa hapa nchini.
Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano ya mashine hiyo pamoja na kufunga rasmi mafunzo ya awamu ya kwanza kwa vijana 15 yaliyosimamiwa na kutekelezwa na kampuni ya Small Enterprise Supplier Development Corporation Tanzania Ltd (SESDCorp), Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Bw. Angelus Ngonyani alisema vifaa hivyo ni sehemu ya jitihada za kuimarisha uwezo wa taasisi za mafunzo ya ufundi stadi hapa nchini ili kuendana na maendeleo ya teknolojia na mahitaji ya soko la ajira.

“Tunawashukuru EACOP na washirika wake kwa msaada huu muhimu. Kupitia teknolojia hii, wakufunzi wetu wamepata mafunzo yanayokidhi viwango vya kimataifa na kuwa tayari kushiriki kikamilifu katika sekta ya nishati pamoja na miradi mingine ya kimkakati,” alisema Bw. Ngonyani.
Aliongeza kuwa maendeleo ya sekta ya nishati na viwanda yanahitaji wataalamu wenye ujuzi wa hali ya juu, hivyo mafunzo hayo yatawawezesha wakufunzi kuongeza ushindani wao katika soko la ajira la ndani na kimataifa.
Aidha, alisema VETA itaendelea kushirikiana kwa karibu na EACOP pamoja na wadau wengine kuhakikisha mafunzo yanayotolewa yanakuwa chachu ya kuwafanya Watanzania kuwa sehemu ya mafanikio ya miradi mikubwa ya maendeleo.
Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa EACOP Tanzania, Bw. Geofrey Mponda, alisema mpango huo ni utekelezaji wa hati ya makubaliano (MoU) iliyosainiwa kati ya EACOP na VETA Dodoma pamoja na vyuo vingine vya VETA nchini, kwa lengo la kutoa mafunzo kwa vijana ili waweze ili waweze kujiajiri au kuajiriwa kuendana na mahitaji ya soko la ndani na kimataifa.
“Kwa mradi wa EACOP, maendeleo ya rasilimali watu ni jambo la msingi kwa kuwa ni sehemu ya wajibu wetu wa kijamii na msingi wa mafanikio ya mradi. Tunaamini ushirikiano huu utafungua fursa zaidi za mafunzo, ajira na maendeleo kwa vijana wa Kitanzania,” alisema Bw. Mponda.
Alisema mradi huo unatambua umuhimu wa kuwekeza kwa vjana wa Kitanzania ili kuwawezesha kupata maarifa, ujuzi na uzoefu kupitia ushiriki wao katika mradi huo na miradi mingine ya kimkakati.
“Kupitia ujuzi walioupata, wataalamu hawa wataendelea kuwajengea uwezo wanafunzi wengine watakaojiunga na vyuo vya VETA, jambo litakaloifanya Tanzania kuwa na wataalamu wengi zaidi wenye uwezo wa kushiriki katika sekta ya nishati,” aliongeza.
Naye Mratibu wa EACOP kutoka Wizara ya Nishati, Bi. Melania Nyimbo, alisema mafunzo hayo yametolewa kwa wakufunzi kutoka taasisi mbalimbali za elimu ya ufundi na teknolojia, vikiwemo vyuo vya DIT, Don Bosco, VETA Dodoma na chuo cha Ufundi Arusha (ATC).
“Sisi kama Serikali tutaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali, ikiwemo EACOP, kuhakikisha sekta ya nishati inatoa mchango stahiki katika kuzalisha wataalamu watakaoiwakilisha vyema Tanzania katika ngazi ya kimataifa,” alisema Bi. Nyimbo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha VETA Dodoma, Bw. Deodatus Orotha, mbali na kuishukuru EACOP kwa msaada huo, alisema mashine hiyo itawasaidia wanafunzi kupata uelewa wa kina kuhusu mbinu za kisasa za uchomeleaji wa mabomba, hususan katika maeneo yanayohitaji usahihi mkubwa na viwango vya juu vya ubora.
“Mashine hii itawapa wanafunzi wetu uzoefu wa vitendo unaokidhi mahitaji ya waajiri wa ndani na wa kimataifa. Hii ni hatua kubwa katika kuimarisha elimu ya ufundi stadi nchini,” alisema Bw. Orotha.
Mmoja wa wahitimu wa mafunzo hayo kutoka Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Bi. Lisa John, alisema mafunzo hayo yamewawezesha kupata ujuzi wa kisasa unaohitajika katika sekta ya nishati na viwanda, huku yakiongeza uwezo wao wa kushindana katika soko la ajira.
“Mafunzo haya yamebadilisha mtazamo wangu kuhusu taaluma ya uchomeleaji inayotumika katika miradi mikubwa ya mafuta na gesi duniani,” alisema Bi. John.
Wanahisa wa mradi wa EACOP ni TotalEnergies yenye asilimia 62; Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini (TPDC) na Kampuni ya Taifa ya Mafuta ya Uganda (UNOC) zinazomiliki asilimia 15 kila moja; huku Kampuni ya Taifa ya Mafuta ya China (CNOOC) ikimiliki asilimia 8 ya hisa za mradi huo.
