Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika ya Mashariki (EACOP) umepongewa kwa kurejesha vizuri mazingira ya asili ya viumbe hai wa baharini, kupanda mikoko na kuotesha mwani katika mwambao wa mkoa wa Tanga.
EACOP inashirikiana na taasisi 10 katika zoezi hilo kwa sababu inajenga temino kwenye Rasi ya Chongoleani kwa ajili ya kuhifadhi mafuta ghafi kwa ajili ya masoko ya kimataifa.
Akizungumza baada ya warsha ya siku mbili ya kurejesha mazingira ya asili ya baharini na kurejesha ajira zinazohusiana na bahari iliyoandaliwa na EACOP Jijini hapa, Afisa Uvuvi wa Mkoa wa Tanga, Gladys Manyika aliishukuru EACOP kwa mradi wa urejeshwaji wa mazingira ya asili ya bahari.
Alisema sasa ni dhahiri kwamba mradi hautaadhiri shughuli za uvuvi bali utakuwa na tija kwa wavuni, kwani mradi ukifikia mahali pazuri itapelekea kuongezeka kwa wingi wa samaki.
“Utekelezaji wa mradi huu mpaka sasa una miaka mitatu. Sasa tuna sababu za kuridhika kwamba mradi hautaathiri shughuli za uvuvi. Aidha maafisa wa EACOP wanakutana na wavuvi mara kwa mara ili kujenga uwelewa wa mradi huu.”
Kiongozi wa nyasibandia, kutoka Shule Kuu ya Sayansi na Teknolojia ya Uvuvi, Dk. Blandina Lugendo, amesema zoezi la kulinda bahari katika mwambao wa Tanga linaendelea.
“Sisi ni wadau katika programu hii. Mradi wetu unaendelea na ni salama kabisa. Nyasi zitavutia samaki wengi kuishi katika eneo hilo na hili litakuwa na jita kwa wavuvi.”
Dk. Lugendo aliwatoa hofu wananchi kwa kusema eneo lililoathirika na mradi na mradi ni dogo wakati eneo linalopandwa nyasi hizo ni kubwa zaidi.
“Mradi huu ukikamilika utaongeza idadi ya Samaki majini kwani mazalia ya Samaki yatakuwa yameongezeka na itakuwa ni faida kwa wananchi na wavuvi wa eneo hilo la Chongoleani,” alisisitiza.
Aidha, Mshauri ya Sayansi ya Baharini wa EACOP (Scientific Marine Advisor), Matthew Richmond alieleza kuridhishwa na kazi inayotekelezwa na EACOP ni kutokana na utafiti mkubwa uliofanywa kuhusiana na nmanma bora ya urejeshwaji wa uoto wa asili wa bahari.
“Hayo yote yanafanywa katika jitihada za kutunza mazingira ya Bahari na viumbe hai vya bahari ilikuendelea kuwa na tija kwa watumiaji wote wa Bahari,” alisema Richmond.
EACOP ina programu ya kulinda mazingira kutokana na shughuli za mradi ambayo inatekelezwa na taasisi 10.
Alieleza kwamba programu ya kulinda mazingira ya habari itaendelea pengine kwa miaka 20 au 30 au zaidi katika eneo hilo.
“Hii itategemea tafiti zinazofanywa wakati huu na za baadaye,” alisema na kuongeza kuwa kazi iliyokwishafanywa itailetea sifa serikali ya Tanzania duniani kwa kulinda vizuri mazingira.
Aidha, aliongeza kuwa miradi inayotekelezwa inatoa ajira kwa Watanzania na ujuzi wa kisasa wa kulinda mazingira ya bahari.