Tarehe 24 Juni 1982, majira ya usiku, ndege ya British Airways aina ya Boeing 747-200, iliyokuwa imebeba abiria 263 ilikuwa ikiruka kwa utulivu takribani urefu wa futi 37,000 juu ya bahari ya Hindi.
Ndege hiyo ilikuwa katikati ya safari ikitokea ikielekea Sydney nchini Australia. Ilipokaribia kufika katika anga la Indonesia Ghafla, injini zote nne zilianza kuzimika moja baada ya nyingine.
Hakukuwa na mlipuko wala onyo la wazi. Ndege hiyo ilikuwa ikiruka hewani bila nguvu ya injini.
Chanzo hakikujulikana mara moja. Lakini ukweli ulikuwa ni kwamba ndege ilikuwa imeingia katika wingu la majivu ya volkano kutoka mlipuko wa Mlima Galunggung nchini Indonesia.
Majivu hayo hayaonekani kwenye rada ya hali ya hewa, lakini yanaweza kuharibu injini kwa haraka sana.
Ndipo Rubani Mkuu, Eric Moody, akatoa tangazo katika hali ya utulivu ambalo litabaki kukumbukwa muda wote katika historia ya matukio ya sekta ya anga, kwa utulivu wake wa kipekee alisikika akisema;
“Abiria mabibi na mabwana, tunakabiliwa na tatizo dogo. Injini zote nne hazifanyi kazi. Tunafanya kila tuwezalo kuziwasha tena. Tuna matumaini hamna wasiwasi mkubwa.”
Kwa takribani dakika 15, Boeing 747 hiyo ilisafiri hewani, ikishuka taratibu gizani kuelekea eneo la Indonesia pasi na injini.
Rubani aliamua kuwa kama injini zisingewaka kabla ya kufikia futi 12,000, wangelazimika kutua baharini.
Katika urefu wa takribani futi 13,500, injini ya nne iliwaka tena. Baadaye nyingine zikafuata. Lakini changamoto haikuishia hapo.
Majivu yalikuwa yamesugua vioo vya mbele vya chumba cha marubani na kupunguza sana uwezo wa kuona. Hivyo, ndege ilitua kwa msaada mkubwa wa vifaa saidizi (instruments) katika uwanja wa Halim Perdanakusuma, Jakarta.
Wahudumu na abira wote 263 waliokuwamo ndani waliokolewa salama.
Rubani Eric Moody alifariki dunia mwezi Machi 2024 akiwa na umri wa miaka 82.
