You are currently viewing Hatua kwa hatua Uchaguzi Mkuu 2025

Hatua kwa hatua Uchaguzi Mkuu 2025

Na Mwandishi Wetu

Uchaguzi Mkuu wa kumchagua Rais, wabunge na madiwani umefanyika nchini, huku kukishuhudiwa misururu ya mamia ya wananchi waliopanga mistari kusubiri kupiga kura.

Licha ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), kutangaza kufungua vituo vya upigaji kura saa 1:00 asubuhi, kabla ya muda huo, tayari wananchi walishafika vituoni kuhakiki majina yao.

Katika vituo hivyo, hakukuwa na malalamiko ya ama kukosekana kwa majina yao au mlolongo mrefu hadi kupiga kura, badala yake ilimchukua mtu si zaidi ya dakika tano kupiga kura na kuondoka.

Uchaguzi huo, unaohusisha wagombea urais 17 kutoka vyama mbalimbali vyenye usajili wa kudumu na wa ubunge 1,735, kadhalika wa udiwani, unafanyika katikati ya mazingira shwari na tulivu.

Ingawa kuna harakati mitandaoni zinazohamasisha wananchi kuacha kupiga kura, lakini uhalisia ni tofauti, mamia ya wananchi wameshuhudiwa wakifurika vituoni kutimiza haki yao ya msingi ya upigaji kura.

Akizungumzia hilo, mmoja wa wapigakura katika Kituo cha Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Kelvin Joseph amesema imemchukua si zaidi ya dakika tano kuhakiki hadi kupiga kura.

Ameeleza alipofika alipokelewa na kupewa ushirikiano kutoka kwa makarani wa uchaguzi, akapewa utaratibu kisha akaelekezwa jinsi ya kupiga kura na akapiga.

“Baada ya kuingia katika chumba cha kupigia kura, nilionyesha kitambulisho kisha akaandika namba yangu na akanipa karatasi na kunihoji maswali kadhaa na nikapiga kura,” amesema Joseph.

Mvua kubwa iliyonyesha katika Kata ya Mtonga, Korogwe Mjini, mkoani Tanga, haikuwa kikwazo kwa wananchi kujitokeza kupigakura. Wapo waliotumia miamvuli na wengine wakikubali kunyeshewa, ilimradi watimize haki hiyo ya kupiga kura.

Mgombea urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt Samia Suluhu Hassan alipiga kura Chamwino jijini Dodoma, huku akiwahamasisha wananchi kuendelea kujitokeza kupiga kura.

Mgombea mwingine wa nafasi hiyo kupitia NRA, Hassan Almasi naye alipiga kura na kusifu namna uchaguzi unavyokwenda, akisisitiza ni wa kwanza kusimamiwa na Tume Huru ya Uchaguzi.

Hakukuwa na mgombea urais aliyepinga uchaguzi huo, kila mmoja alisifu utaratibu unavyokwenda na kueleza anasubiri kwa hamu matokeo.