Uchapakazi, weledi na heshima ya Rais, Dkt Samia Suluhu Hassan katika uongozi, ilianza kuonekana mapema tangu alipokuwa Makamu wa Rais, kama ilivyowahi kusimuliwa na mtangulizi wake, hayati Dkt John Magufuli.
Dkt Magufuli, ambaye leo inaadhimishwa miaka mitano tangu kifo chake, Machi 17, 2021 alilithibitisha hilo, mbele ya Mkutano Mkuu wa CCM, uliofanyika mwaka 2020, aliposema Dkt Samia ni mchapakazi na mwenye heshima.
Katika hotuba yake pindi alipoteuliwa na CCM kuwa mgombea urais 2020, alisema Dkt Samia ni mchapakazi na mwenye heshima na kwamba kila alipomtuma alikwenda kufanya kazi kama ilivyopaswa.
“Nilipomchagua Mama Samia kuwa mgombea mwenza mwaka 2015, sikuujua vizuri uchapakazi wake wakati ule, lakini mama huyu nasema kwa dhati bila unafiki ni mchapakazi, ana heshima, kila nikimtuma anaenda, kwa hiyo nimeamua tena Mheshimiwa Samia ndio awe mgombea mwenza katika kipindi cha miaka mitano.”
