You are currently viewing TAMISA inavyochagiza utoaji huduma katika sekta ya madini nchini

TAMISA inavyochagiza utoaji huduma katika sekta ya madini nchini

NA FLORID MAPUNDA, Dar es Salaam

Ni dhahiri kuwa kuanzishwa kwa Chama cha watoa huduma na wasambazaji bidhaa migodini (TAMISA) kunasaidia kutoa nafasi kwa Watanzania kushiriki kikamilifu  katika utoaji wa huduma na usambazaji bidhaa kwenye sekta ya madini hapa nchini.

Uanzishwaji wake umechangia kutoa fursa kwa Watanzania kufaidika na rasilimali zao chini ya uongozi mahiri wa Rais Samia Suluhu Hassan. 

Katika makala hii mwandishi anajaribu kuangazia malengo na matarajio mapana  ya Tamisa katika kuwezesha Watanzania kutoa na mchango wao stahiki katika sekta hii.

Mwenyekiti wa Chama cha Wasambazaji wa Sekta ya Madini Tanzania (TAMISA), Bw.  Peter Kumalilwa, akizungumza na Rais na Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Barrick Gold Corporation, Bw. Mark Bristow, wakati mwenyekiti huyo alipotembelea ofisi za Barrick jijini Dar es Salaam, hivi karibuni.

Kuundwa kwa TAMISA kunaenda kufungua milango kwa wadau wote wa sekta ya madini kama vile wachimbaji wakubwa kwa wadogo, wauzaji wakubwa kwa wadogo, lakini pia wauza vifaa vya kuchimba madini pamoja na teknolojia ambayo hutumika sana katika migodi ya nchi za dunia ya kwanza. Teknolpojia hii itawasaidia watanzania wengi kunufaika kupitia sekta hii.

Ifahamike kwamba Tanzania tuna kiasi kikubwa cha migodi ya madini na karibu kila mkoa kuna migodi ya kutosha, na wachimbaji wengi wa kitanzania huchimba kwa kutumia mbinu za kizamani hivyo inawawia ugumu kugundua mkondo wenye madini, hivyo kuundwa kwa TAMISA kutawasaidia wachimbaji wadogo kupata elimu sahihi na kuweza kutumia vifaa bora vya kisayansi vyenye tija katika kazi zao za uchimbaji.

Vifaa vingine ambavyo vinakuja kama zao la TAMISA ni pamoja na vifaa vya uchunguzi ambavyo vnya kazi hii kwa uhakika tofauti  na hapo awali ambapo mtaguindua sehemu uenye madini, hivyo itapelekea watanzania kunufaika kupitia sekta hii ya madini. 

Ni kwa muda mrefu Tanzania hatukuwa na chama cha aina hii chenye msaada kwa wadau wake wote wa madini hususani kwa ajili ya kutoa huduma kwa wadau wa sekta ya madini na hivyo ujio wa tamisa utaleta mapinduzi makubwa kwa Watanzania na kuona tija kupitia sekta hii.

Kabla ya kuanzishwa kwa chama hicho, Mwenyekiti wake, Bw. Peter Kumalilwa amebainisha kwamba kulikuwa na ukosefu wa uwakilishi wa kuunga mkono ustawi wa kijamii na kiuchumi wa wadau hawa, hivyo kupelekea kukosa taarifa muhimu na msaada wa kitaaluma na kitaalamu hasa wa kisayansi katika ulimwengu huu wa sasa wa sayansi ya Teknolojia, ambapo shughuli nyingi hufanywa kwa kuzingatia taaluma ya juu ambayo hutumika sana katika migodi mbalimbali ya kimataifa.

Kutokana na taarifa iliyotolewa na Bw. Kumalilwa ni kwamba chama hiki kitakata kiu ya wadau wote katika sekta ya madini na kukidhi hitaji muhimu la sauti ya pamoja na rasmi kwa watoa huduma na wasambazaji hivyo kufunga pengo hili kwa kushughulikia changamoto zinazokabili sekta na kukuza ushirikiano kati ya wanachama, serikali, na taasisi za kibinafsi.

“Hiki chama kimekuwa ni imara kuitokana na waanzilishi wake wote kuwa ni watu muhimu wa sekta hii ambao ni kundi la wataalamu wenye uzoefu na wadau ndani ya sekta ya madini. Hii inajumuisha wasambazaji, watoa huduma, na wafuasi wa maudhui ya ndani”. Amebainisha Bw. Kumalilwa.

Kutokana na taarifa iliyotolewa na Tamisa ni kuwa, idadi ya wanachama inaendelea kuongezeka ambao ni wasambazaji wa vifaa na watoa huduma ambao wanatambua umuhimu wa kuwa na jukwaa lililoungana kushughulikia changamoto na fursa.

Ni mwaka mmoja tu tangu kuanzishwa kwake, lakini mpaka sasa kimekuwa ni Chama maarufu na kimekwisha shughulikia kero kadha wa kadha ambazo zilikuwa zinawakabili wadau wa sekta ya madini kama vile upatikanaji wa vifaa maalumu vya uchimbaji na vya kisasa.

Kwa upande wa aina ya Uanachama Bw. Kumalila alibainisha uwepo wa aina mbalimbali za uanachama katika makundi matatu ya ambayo ni uanachama wa kawaida, shirikishi, na uanachama wa heshima.

Kuna makundi haya matatu ya uwanachama hasa kuhakikisha ushirikishwaji na uwakilishi kati ya wadau tofauti katika sekta hiyo. Muundo huu unaruhusu Tamisa kutimiza mahitaji tofauti ya wanachama wake huku ikitumia utaalamu na mtazamo wa kipekee wa kila kundi.

Majukumu mengine ya Tamisa ni pamoja na kutoa utetezi, uimarishaji wa uwezo, na huduma za mtandao. Pia inarahisisha upatikanaji wa rasilimali na taarifa zinazowezesha uwezo wa wanachama wake.

Kwa upande wa kutoa huduma za Utetezi, Bw. Kumalilwa amesema wameingia ubia na taasisi mbalimbali za kisheria kwa lengo la kuwasaidia wanachama wao pale ambapo wanakubwa na masuala ya kisheria na wanashindwa kuyatatua wenyewe, hivyo kwa sasa watakuwa wamepata msaada mkubwa na kuwaongezea nguvu ya ufanyaji kazi wao.

Mafanikio mengine ambayo Bw. Kumalilwa alieleza yamepatikana ndani ya kipindi kifupi cha utawala wake ni pamoja na kupata kundi kubwa la watoa huduma ambao ni Wasambazaji wanaotoa bidhaa na huduma muhimu kwa shughuli za madini, kama vile vifaa, usafirishaji, mavazi ya wachimbaji pamoja na vifaa vya umeme kama vile betri, tochi na vifaa vya kuchajia, wasambazaji wa vyakula, huduma za kisheria, bima, na ushauri.

Pamoja na hayo Tamisa imejipanga kuendelea kutimiza dhamira yake ya kujihusisha na utetezi wa sera, inashiriki katika majukwaa ya wadau, na inashirikiana na wahusika muhimu wa serikali na sekta binafsi ili kuhakikisha kwamba maslahi ya wanachama wake yanazingatiwa katika mchakato wa uamuzi.

Pia inafanya kazi ya kuboresha mazingira ya kisheria na kuimarisha sera za maudhui ya ndani kwa tija ya Watanzania.

Tamisa imejidhatiti katika kuhakikisha inatatua changamoto zote zinazowapata wadau wote walio katika mzunguko wa sekta hii ya madini na ni haki yao kuhudumiwa.

Pamoja na mafanikio ambayo Bw. Kumalilwa ameelezea hakusahau kuelezea kuwepo kwa changamoto na kuahidi kuzitafutia suluhisho.

“mojawapo ya njia ya kupunguza changamoto hizi ni pamoja na kuwezesha warsha juu ya kuzingatia sheria kwa wasambazaji, kusaidia wanachama kuelewa michakato ya manunuzi, na kutoa mafunzo juu ya kufuata kanuni za maudhui ya ndani”. Amebainisha Bw. Kumalilwa.

Hata hivyo amesema anataka kuona uwazi wa utendaji kazi hasa katika utangazwaji wa zabuni na kusisitiza kuwa, ”zabuni ni muhimu kwa wanachama wetu, tunataka uwazi na tunataka kuona mambo yakifanyika kwa njia sahihi ili wanachama waweze kufaidika na fursa hizi kwa urahisi”.

Miongoni mwa mambo ambayo Bw. Kumalilwa alipenda washiriki wa mkutano wafahamu ni pamoja na mafanikio ya taasisi hiyo ambapo alisema imefanya hatua muhimu katika kipindi kifupi. Kumekuwa na ongezeko la idadi ya wanachama, pia amesema wamefanya utetezi mzuri wa taratibu za manunuzi za haki.

“Na nichukue nafasi hii kuongeza, kuwa na eneo kwenye Mkutano wa Uwekezaji wa Kimataifa wa Madini katika Kituo cha Mikutano cha Julius Nyerere, Dar es Salaam, ilikuwa hatua kubwa iliyowakutanisha wadau kutoka mnyororo wa thamani wa madini kuelewa uwepo wetu na kutafuta uwanachama”. Amekiri Bw. Kumalilwa

Pamoja na hayo Bw. Kumalilwa amekiri uwepo wa ushirikiano wa kutosha kati ya Tamisa na Taasisi za Sekta Binafsi Tanzania na Chama cha Madini. Ushirikiano huu unaruhusu Tamisa kutetea kwa ufanisi maslahi ya wanachama wake na kuchangia katika malengo makubwa ya sekta kwa kutumia rasilimali na utaalamu wa pamoja.

Septemba 14, 2024, waziri wa Madini Bw. Anthony Mavunde alialikwa kuzindua chama hicho pamoja na masuala mengine alisema kuwa Serikali ya Tanzania inatoa kipaombele kwa wawekezaji na wazalishaji wa madini wa ndani pamoja na kuhimiza kutumia malighafi zinazozalishwa nchini kwa lengo la kuunga mkono viwanda vya ndani.

Bw. Mavunde alisema kwa kufanya hivyo anaamini makampuni ya wazawa yatakuwa na kuanzisha viwanda vikubwa vitakavyozalisha bidhaa nzuri na pendwa kwa watanzania na kwa kufanya hivyo itapunguza utegemezi wa vifaa vya nje.

Bw. Mavunde hakusita kusifu juhudi zilizofanywa na waanzilishi wa Tamisa pamoja na viongozi wao kwa kujali maslahi mapana ya watanzania na sio maslahi yao binafsi kwani Tamisa inaenda kuunganisha wadau wote wa madini kwani wao wote wana mahitaji yanayofanana hivyo changamoto zao zote zitatatuliwa kupitia chama hicho.

“Naamini Tamisa itaisaidia Serikali kwa kiasi kikubwa kutatua changamoto ambazo zitaainishwa na kila mdau wa madini ataona thamani ya kuwa kwenye sekta hii” amesema Bw. Mavunde.

Kupitia hafla hiyo ya uzinduzi wa Chama hicho Bw. Mavunde alikiri kuwa Serikali iko tayari inafurahia kuona watanzania wanafanikiwa kwa kufanya kazi na kujipatia kipato, hivyo mafanikio ya watanzania ndio mafanikio ya Serikali pia.

Hapo awali watanzania wengi walikuwa wanachimba madini kienyeji na kutoona faida ya kazi hiyo lakini kupitia Tamisa wachimbaji wengi watapata kufahamu mbinu bora za uchimbaji, namna ya kupata vifaa bora na vya kisasa, namna ya kupata mikopo yenye riba nafuu kwa ajili ya shughuli zao za uchimbaji na hata uuzaji wa madini hayo.

Mnamo Mwezi Oktoba 2024, Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Samia akiwa kwenye maonesho ya madini Mkoani Geita alisema katika ripoti ya mwaka 2023, sekta ya madini ilifanikiwa kuingiza kiasi kikubwa cha fedha za kigeni ambapo iliingiza asilimia 56 ya fedha zote zilizoingia nchini.

Hapo ndio tunaona ni namna gani sekta ya madini inavyotoa mchango mkubwa kwa serikali na kwa watanzania kwa ujumla wake, hivyo ujio wa Tamisa utaendelea kufungua milango Zaidi kwa wafanyabiashara wakubwa kwa wadogo kuchangamkia fursa hii ya madini.

Kwa Makala haya tunaipongeza Serikali kupitia kwa Waziri wa Madini Bw. Anthony Mavunde kwa kuwa bega kwa bega na Tamisa na kuunga mkono jitihada zinazofanywa. Lakini pia kwa kutenga fedha kwa ajili ya kuwakopesha wafanyabiashara wa madini.

Hata hivyo Wizara ya madini imefanikiwa kujenga masoko mbalimbali ya uuzaji wa madini, kitu ambacho kitaisaidia Watanzania kuuza madini yao kwa urahisi zaidi na kwa ushindani. Baadhi ya mikoa ambayo serikali imejenga masoko hayo ni pamoja na Ruvuma katika wilaya ya Tunduru, Dodoma, Geita, Mwanza, Manyara, mkoa wa Mara na mkoa wa Arusha.

Leave a Reply