You are currently viewing Kanisa Katoliki lapiga marufuku watawa kujihusisha na kampeni za siasa
Askofu wa Jimbo Katoliki la Lindi, Mhashamu Wolfgang Pisa

Kanisa Katoliki lapiga marufuku watawa kujihusisha na kampeni za siasa

Kanisa Katoliki nchini limeweka marufuku kwa watawa wa kike na kiume na kiongozi yeyote wa Kanisa Katoliki kujihusisha na kampeni za siasa au kutambulishwa na chama chochote cha kisiasa kama mshirika wao. Pia wamekumbushwa kwamba jukumu lao ni kuinjilisha kadiri ya wito wao.

Katazo hilo limetolewa leo Septemba 25, 2025 na Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) ambaye pia ni Askofu wa Jimbo Katoliki la Lindi, Mhashamu Wolfgang Pisa O.F.MCap. wakati wa Adhimisho la Misa Takatifu ya kilele cha Jubilee ya miaka 100 ya Seminari Kuu ya Mt. Paulo Mtume Kipalala Jimbo Kuu Katoliki la Tabora.

Askofu Pisa amesema kuwa haitaruhusiwa kwa mtawa yeyote au mseminari katika mazingira yeyote yale atakayeruhusiwa kujihusisha na jambo lolote lenye taswira ya kisiasa hata kama mtawa angekuwa na ndugu mwenye kujihusisha na siasa.

Pia amekea watu kuwarubuni watawa na kuwahadaa ili washiriki kampeni hizo na kusisitiza kuwa hiyo ni dhambi.

“Mnakatama mseminari, unamsomba tu wakati hata hajui kinachoendelea wala redio hasikilizi, hiyo ni dhambi pia,” amesema Mhashamu Pisa na kuonya wasilete unajisi kwenye kanisa.