Morogoro: Februari 15; Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, ameionya kampuni ya Henan Railway ya China inayotekeleza ujenzi wa barabara ya Ifakara–Mbingu (km 62.5) kuwa Serikali haitasita kuvunja mkataba wake na kuipendekeza iwekwe kwenye orodha ya wakandarasi watakaopigwa marufuku kushiriki zabuni za miradi ya Serikali ikiwa itaendelea kushindwa kutekeleza wajibu wake kwa mujibu wa mkataba.
Onyo hilo amelitoa wakati wa ukaguzi wa maendeleo ya mradi huo mkoani Morogoro, ambapo alieleza kutoridhishwa na kasi ya ujenzi, akibainisha kuwa haikidhi matarajio licha ya Serikali kuwa tayari imetoa malipo ya awali kwa mkandarasi.
Ulega alisema Serikali haiwezi kuendelea kuvumilia ucheleweshaji wa utekelezaji wa miradi ya kimkakati inayogusa maisha ya wananchi na maendeleo ya uchumi wa taifa.
“Hivi hamuoni namna wananchi wanavyoumia kwa kutotimiza wajibu wenu kwa mujibu wa mkataba? Barabara haijengwi kwa kasi, vumbi ni jingi na usumbufu kwa wananchi ni mkubwa. Hili hatuwezi kuvumilia. Mkiendelea hivi italazimika kuchukua hatua ngumu,” alisema Waziri Ulega.
Kutokana na hali hiyo, Waziri huyo ametoa muda wa wiki moja kwa wataalamu wa Wizara ya Ujenzi na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kukutana na uongozi wa juu wa kampuni hiyo katika kikao cha ngazi ya juu ili kujadili hatma ya utekelezaji wa mradi huo.
Alieleza kuwa hadi sasa mradi umefikia takribani asilimia tano pekee ya utekelezaji, licha ya Serikali kuwa tayari imelipa Shilingi bilioni 9.5 kama malipo ya awali. Kwa mujibu wa Waziri huyo, kiwango hicho cha maendeleo hakilingani na fedha ambazo tayari zimetolewa.
“Serikali haitakuwa tayari kuona fedha za umma zinatumika bila kuleta matokeo yaliyokusudiwa. Mkandarasi lazima aonyeshe uwezo na dhamira ya kukamilisha mradi huu kwa wakati, vinginevyo hatua stahiki zitachukuliwa,” alisisitiza.
Aidha, Ulega amesema Serikali imejipanga kuhakikisha barabara hiyo inakamilika kwa wakati ili kupunguza adha wanazokumbana nazo wananchi kutokana na ubovu wa miundombinu, ikiwemo usumbufu wa usafiri, vumbi na kuongezeka kwa gharama za usafirishaji na nauli.
