ZAIDI ya wakazi 7,678 wa kata ya Mwamabanza iliyopo wilaya ya Magu mkoani Mwanza wanatarajiwa kupata huduma ya maji safi na salama kuanzia Juni mwaka huu.
Hayo yameelezwa jana tarehe 15 Mei, 2025 na Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Magu, Mhandisi Daudi Amlima katika ziara ya Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Magu, Simon Mpandalume aliyetembelea vijiji vya Mwamabanza, Mwalinha na Salong’we.
Ziara hiyo ililenga kufuatilia maendeleo ya miradi inayotekelezwa katika kata hiyo, kusikiliza kero za wananchi na kutatua changamoto mbalimbali za kijamii.

Akizungumza na wananchi vijiji hivyo kwa nyakati tofauti, Mpandalume ambaye alimpigia simu meneja huyo wa RUWASA – Magu mbele ya mikutano yake, amewaomba wananchi hao kuwa na subira kwa kuwa changamoto iliyokuwa imekwamisha maji kusambazwa katika kata hiyo ni pampu ambazo tayari zimepatikana tatu.
Naye Mhandisi Amlima amesema mradi huo umefikia asilimia 90 hivyo ni uhakika kwamba kuanzia mwezi ujao, wataanza majaribio ya usambazaji wa maji kwa wananchi.
Amesema baada ya kupata pampu hizo, kazi inayofuata ni kupeleka umeme katika chanzo cha maji Bugabu ili uweze kuwasha pampu hizo.
Pamoja na mambo mengine, Mwenyekiti huyo amewaahidi wananchi hao kuwa barabara ya Mwamabanza- Salong’we- Mwalinha – Nyamwigamba utaendelea hivi karibuni baada ya mvua kukatika kwa sababu tayari mkandarasi ameshapewa fedha za kutengeneza barabara hiyo kwa kiwango cha changarawe.