Kiongozi Mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei ameuawa katika shambulio kubwa dhidi ya Iran lililofanywa na Israel na Marekani, imesema televisheni ya taifa. Maafisa kadhaa waandamizi pia wameuawa.
Kifo hicho kimetilia shaka mustakabali wa Jamhuri hiyo ya Kiislamu na kuongeza hatari ya kutokuwa na utulivu wa kikanda.
Rais Donald Trump wa Marekani alitangaza kifo hicho saa kadhaa kabla, akisema kinawapa Wairan fursa kubwa ya kuichukua nchi yao.
Televisheni ya serikali iliripoti kwamba kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 86 aliuawa katika shambulio la anga lililolenga makazi yake katikati mwa jiji la Tehran. Picha za satelaiti kutoka kampuni ya Airbus zilionyesha kuwa eneo hilo lililipuliwa kwa mabomu mengi.
Kifo chake ofisini kwake kilionyesha kwamba alisimama miongoni mwa watu na kuwa mstari wa mbele katika majukumu yake, akikabiliana na kile ambacho maafisa wanakiita kiburi cha kimataifa, ilisema televisheni ya taifa.
“Khamenei, mmoja wa watu waovu zaidi katika Historia, amekufa,” Trump aliandika kwenye mtandao wa kijamii.
Alionya kuhusu “mashambulizi makali ya mabomu na ya uhakika” ambayo alisema yataendelea wiki nzima na hata zaidi, ikiwa ni sehemu ya operesheni kali ambayo Marekani imehalalisha kwa kusema ni muhimu ili kuangamiza uwezo wa nchi hiyo kuwa na zana za nyuklia.
Maafisa waandamizi pia waliuawa
Shirika la habari la serikali – IRNA pia liliripoti vifo vya mkuu wa jeshi la Iran la Walinzi wa Mapinduzi na mshauri mkuu wa Khamenei kuhusu usalama.

Meja Jenerali Mohammad Pakpour alichukua nafasi ya kamanda mkuu wa Walinzi wa Mapinduzi baada ya Israel kumuua kamanda wake wa zamani katika vita vya siku 12 Juni iliyopita.
Mshauri huyo, Ali Shamkhani, kwa muda mrefu amekuwa kiongozi mkuu katika taasisi ya usalama ya Iran.
Aidha jamaa kadhaa wa Khamenei pia waliuawa, akiwemo binti yake, wakwe zake, wa kike na kiume na mjukuu.
Iran, ambayo ilijibu mashambulizi hayo kwa kufanya mashambulizi yake,ilionya kuwa italipiza kisasi, huku Baraza la Mawaziri likisema kwamba “uhalifu huu mkubwa hautakwenda bila kujibiwa.”
Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi limetishia kuanzisha “operesheni yake kali zaidi ya mashambulizi” kuwahi kushuhudiwa ikilenga kambi za Israel na Marekani.
Baraza la mpito laundwa
Iran imeunda haraka baraza la kutawala nchi hadi kiongozi mpya mkuu atakapochaguliwa. Linaongozwa na Rais Masoud Pezeshkian na wajumbe wengine wawili waandamizi.
Mkuu wa Idara ya mahakama na mwenye msimamo mkali Gholamhossein Mohseni Ejei pia ni sehemu ya watatu hao, televisheni ya serikali iliripoti ikimnukuu Mohammad Mokhber, mmoja wa washauri wa Khamenei.
Ingawa baraza hili litaongoza katika kipindi cha mpito, jopo la wanachama 88 linaloitwa Baraza la Wataalamu linatarajiwa kumchagua haraka kiongozi mpya mkuu chini ya sheria ya Iran.

Awali, ripoti kuwa Khamenei alikuwa ameuawa zilizusha shangwe mjini Tehran. Watu katika mji mkuu huo walisikika wakipiga kelele kwa furaha kutoka madirishani mwao huku habari zikisambaa kupitia vyombo vya habari vya Iran vilivyoko uhamishoni ambavyo vinaweza kupokelewa nchini humo kwa setilaiti.
Lakini kwa upande mwingine, waombolezaji walisimika bendera nyeusi ya maombolezo juu ya kaburi la Imam Reza huko Mashhad, jiji la pili kwa ukubwa nchini Iran na eneo kubwa la hija kwa Waislamu wa Kishia.
Mashambulizi yaendelea
Milipuko kadhaa mikubwa ilisikika kwa siku ya pili Jumapili katika eneo la kitovu cha biashara cha kikanda Dubai na katika mji mkuu wa Qatar wa Doha, mashahidi walisema, baada ya Iran kuanzisha mashambulizi ya kulipiza kisasi dhidi ya mataifa jirani ya Ghuba kujibu mashambulizi hayo.
Ving’ora vya kutahadharisha kuhusu mashambulizi ya angani vilisikika mara kwa mara kote Israel mapema Jumapili, huku mfululizo wa milipuko ukisikika huko Tel Aviv nao mfumo wa ulinzi wa anga wa Israel ukijaribu kuzuia makombora ya hivi karibuni ya Iran.
