You are currently viewing Lema atakiwa kuripoti polisi

Lema atakiwa kuripoti polisi

Jeshi la Polisi limetoa ufafanuzi kuhusu taarifa zinazosambazwa na vyombo vya habari ikiwemo kukamatwa kwa watu saba katika mazingira ya kutatanisha tukio ambalo limetajwa kuwa ni ukandamizaji pamoja na taarifa ya kutishiwa maisha ya Godbless Lema.

Taarifa ya ufafanuzi ya Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) David Misime, iliyotolewa leo Ijumaa ya Oktoba 17, 2025 imeeleza kuwa taratibu za kisheria zilifuatwa wakati wa kuwakamata watuhumiwa kutokana na ushahidi uliokusanywa kabla ya kukamatwa kwao.

“Ushahidi uliokusanywa kabla ya kukamatwa kwao unahusiana na mtuhuma mbalimbali za kihalifu ikiwemo matumizi mabaya ya mitandao kwa kufanya uchochezi, kuhamasisha maandamano ambayo ni kinyume cha sheria na uvunjifu mwingine wa sheria za nchi.” Imeeleza taarifa hiyo.

Watuhumiwa walioshikiliwa wametajwa kuwa ni pamoja na Chief Adronius Kalumuna, Paulo Shijason Musisi, Daniel Damian Lwebugisa, Egbert Aloyce Kikulega, Ramadhan Fadhiri, pamoja na Baziri Waziri.

Pia, jeshi la polisi limesema linafuatilia kwa ukaribu taarifa ya Godbless Lema ambaye aliandika taarifa na kuisambaza kupitia mitandao ya kijamii kuwa maisha yake yapo hatarini na limemtaka kufika kituo cha polisi na kuwasilisha taarifa zake ili taratibu nyingine za kisheria ziweze kuchukuliwa.

Kufuatia matukio hayo mawili, jeshi la polisi limetoa wito kwa wananchi kuendelea kuzingatia taratibu za kisheria kwa kuwasilisha taarifa sahihi kwa jamii na Mamlaka za Haki Jinai ili kuepusha upotoshaji na taharuki zisizo za lazima.

Leave a Reply