You are currently viewing Lissu ambwaga Mbowe uenyekiti Chadema

Lissu ambwaga Mbowe uenyekiti Chadema

KADA machachari wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu ameibuka mshindi katika nafasi ya Mwenyekiti wa chama hicho katika uchaguzi uliofanyika kuanzia jana hadi leo asubuhi kwenye ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.

Lissu ambaye alikuwa Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, alikuwa anachuana na Freeman Mbowe aliyekuwa anatetea kiti hicho.

Hata hivyo, katika ujumbe wake aliouchapisha leo asubuhi kwenye akaunti ya mtandao wa X (zamani Twitter)Mbowe amempongeza Lissu kwa ushindi huo.

“Nimepokea kwa mikono miwili maamuzi ya uchaguzi wa Mkutano Mkuu wa Chama chetu CHADEMA uliohitimishwa leo asubuhi 22 Januari 2025. Nampongeza Mhe. Tundu Lissu na wenzake kwa kuaminiwa kutwikwa jukumu la Uongozi wa Chama. Nawatakia kila la kheri katika kukipeleka mbele Chama chetu,” ameandika Mbowe.

Kwa pongezi hizo za Mbowe kwa Lissu sasa ni ishara tosha kuwa safari ya uenyekiti ndani ya Chadema, imefikia tamati baada ya kuongoza chama hicho kwa miaka 21.

Kwa mujibu wa Katiba ya Chadema, Mbowe atasalia kuwa Mjumbe wa kamati kuu ya chama hicho, huku Lissu akielekea kuunda safu yake mpya ya uongozi kwa kushirikiana na Makamu wake, John Heche ambaye naye anatarajiwa kutangazwa mshindi katika nafasi hiyo.

Leave a Reply