You are currently viewing Magu yajipanga kuelekea mvua za  el nino, wananchi watakiwa kuhama mabondeni

Magu yajipanga kuelekea mvua za  el nino, wananchi watakiwa kuhama mabondeni

KATIKA kutekeleza agizo la Rais Samia Suluhu Hassan kwamba maeneo yenye historia ya mafuriko kuchukua hatua mapema ili kupunguza madhara ya mvua za El nino, Halmashauri ya wilaya ya Magu imetangaza mkakati maalumu unaolenga kulinda usalama wa watu, kuboresha miundombinu na uhifadhi wa chakula.

Pia imebainisha mikakati itakayotekelezwa kwa upande wa afya na elimu pindi mvua hizo za El nino zitakapoanza ili zisiathiri utoaji wa elimu wala huduma za afya.

Hatua hiyo imekuja baada ya utabiri uliotolewa Agosti 18 mwaka huu na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), kuonesha uwezekano wa kutokea kwa El Niño yenye nguvu sawa na ile iliyotokea mwaka 1950.

Akitangaza mkakati huo leo Alhamisi katika kikao cha Kamati elekezi ya maafa wilaya, Mkuu wa Wilaya ya Magu, Jubilate Lawuo amesema mkakati huo ulioandaliwa kwa kushirikiana na Kitengo cha Mipango cha Halmashauri, TANROAD, TARURA, RUWASA, mashirika na wadau wengine unalenga pia kutoa elimu kwa jamii kuhusu athari za mvua hizo.

Amesema kupitia mkakati huo, sasa wilaya imejielekeza katika utekelezaji wa shughuli ambazo zinalenga kuepuka na kupunguza madhara ya mvua za El nino.

Ametaja mikakati hiyo kuwa mbali na kutoa elimu kwa wananchi namna ya kujihadhari, pia ametoa wito kwa wananchi wanaoishi maeneo hatarishi ‘’mabondeni” kuhama. Pia ameunda kamati za maafa katika maeneo yote yanayoweza kukumbwa na mafuriko ili kurahisisha upatikanaji wa taarifa kwa wakati.

“Tumeagiza wataalaam wetu kutenga maghala yatakayotumiwa na wananchi wanaoishi maeneo hatarishi kuhifadhi vyakula vyao, lakini pia maeneo hatarishi kwenye shule zetu yaainishwe, vilevile kuwepo na dawa za kutosha na vifaa tiba kukabiliana na magonjwa ya mlipuko.

“Tunatarajia pia kufuatilia maagizo tuliyotoa kwa Tanroad na Tarura kuhusu kuzibua mitaro ya barabara, madaraja na marekebisho tuliyoagiza katika miundombinu yote ili shughuli myingine za kijamii zisiathiriwe,” amesema.

Awali Mwenyekiti wa Halmashauri, Mhandisi Edward Kihamba amesema tayari baraza la madiwani limebainisha maeneo yote hatarishi na kuunda ushirikiano wa kimkakati kuanzia ngazi ya chini ya kitongoji ili kuepuka madhara hayo.

Pia aliisisitiza TARURA na Tanroad kuharakisha marekebisho ya maeneo yenye miundombinu ambayo inaweza kukumbwa na mafuriko.

Aidha, akiwasilisha taarifa ya mkakati huo kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri, Afisa Mipango wa halmashauri hiyo, Kiiza Malisiale amesema tayari wamebainisha maeneo yaliyopo katika vijiji 26 na vitongoji 56 ni hatarishi hivyo upo uwezekano wa kutokea mafuruko.

Amesema halmashauri tayari imeanzisha mfumo wa utayari wa haraka wa kukabiliana na athari kupitia Kamati za Maafa katika ngazi tofauti za kiutawala. Mkakati huo unalenga kuhakikisha watu wanapata msaada wa haraka na kurudi kwenye maisha yao ya kawaida iwapo kutatokea athari.

Ikumbukwe kuwa Mwanza ni moja ya mikoa 14 ambayo imetajwa kuwa katika hatari zaidi ya kukumbwa na madhara ya El Niño.

Mikoa mingine ni pamoja na Kagera, Geita, Shinyanga, Simiyu, Kigoma, Dar es Salaam, Tanga, Pwani, Morogoro, Mara, Arusha, Kilimanjaro na Manyara.