Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdullah amekabidhi hundi yenye thamani ya Sh Milioni 75 iliyotolewa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ikiwa ni Programu ya mikopo kwa Makundi Maalum Wanawake,Vijana na Walemavu.
Makamu wa Pili wa Rais Hemed amefanya makabidhiano hayo jana Oktoba 31 Mkoa wa Kaskazini Pemba wakati wa Kongamano lililoandaliwa na Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Jumuiya ya CCM la kumpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi kwa uongozi wake wenye mafanikio makubwa katika kipindi cha Miaka Minne.
Hemed amesema miradi mbali mbali inayoendelea kujengwa na Serikali kwa Unguja na Pemba ambayo imemgusa kila mwanachi wa Zanzibar hivyo ipo haja na hoja ya kuendelea kuyatangaza mazuri yanayofanywa na viongozi wakuu wa nchi.
Nae Makamu Mwenyekiti wa UWT Ndg. Zainab Khamis Shomari amesema Utekelezaji wa Ilani katika kipengele cha kuwawezesha wanawake kimetekelezwa kwa kiasi kikubwa ambapo wanawake wamekuwa wakinufaika kupitia program mbali mbali zinazotekelezwa na Serikali za kuwawezesha wananchi kiuchumi.
Mkamu Zainab amesema UWT imejipanga kuwafikia na kuwawezesha wanawake wengi wa Zanzibar kwa kuwapatia mikopo yenyenye Thamani ya Shilingi Milioni 75 zitakazotolewa kwa wanawake wa Mkoa wa kaskazini Pemba ambapo Milioni 170 zitatolewa kwa Pemba nzima.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa UWT Ndg. Suzan Peter Kunmabi (MNEC) amesema Serikali ya Awamu ya Nane imefanya mambo mengi ambayo yanawanufaisha wanawake katika nyanja mbali mbali za kiuchumi na kijamii ndani ya Zanzibar.