You are currently viewing Mkurugenzi NMB awafunda wahitimu ‘Form Four’ Charlotte Sekondari

Mkurugenzi NMB awafunda wahitimu ‘Form Four’ Charlotte Sekondari

Na Mwandishi Wetu, Morogoro

KUELEKEA mitihani ya Taifa ya Kidato cha Nne itakayofanyika Novemba 11, 2024, wahitimu wa Shule ya Sekondari Charlotte iliyopo Tungi Mkwajuni, Manispaa ya Morogoro, wametakiwa kumtanguliza Mungu, kuwa na nidhamu, bidii, uadilifu na uaminifu, ili kupata mafanikio zaidi kielimu, kimaisha na kiimani.

Wito huo umeetolewa na Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna, wakati wa Mahafali ya 12 ya shule hiyo inayomilikiwa na Shirika la Masista wa Kazi ya Roho Mtakatifu, yaliyofanyika Jumamosi Oktoba 12, yaliyohudhuriwa pia na menejmenti ya benki hio.

Mahafali hayo yalitanguliwa na Misa Takatifu iliyoongozwa na Padre Isdory Ndekumanya wa Shirika la Mapdre wa Maisha ya Kitume wa Kazi ya Roho Mtakatifu, aliyemuongoza mgeni rasmi Zaipuna kukata utepe kuzindua Maktaba Mpya ya shule hiyo yenye usajili namba; S.4445.

Akizungumza wakati wa hotuba yake, Zaipuna aliiishukuru Bodi ya Shule hiyo yenye wanafunzi 462 kumpa heshima ya kuwa mgeni rasmi wa tukio hilo, lililomrejeshea kumbukumbu za miaka 33 iliyopita alipokuwa akihitimu Kidato cha Nne katika Sekondari ya Kilakala mjini Morogoro.

“Kila mtu anayo safari yake ya kimaisha, lakini historia za maisha ya wengine zina kitu cha kujifunza kinachoweza kukusaidia nawe, kwa hiyo mnapohitimu kidato cha nne leo, kila mmoja wenu amepiga hatua, hivyo niwaombe muendelee kumtumikia na kumtumainia Mungu na kuweka juhudi katika kila mnachofanya.

“Nimepitia hatua mbalimbali za kielimu tangu hapo, baadaye maisha ya ajira na kama nilivyosema, kila mmoja ana safari yake, na katika safari yangu kielimu na kimaisha, vitu vilivyonisaidia kupata mafanikio ni pamoja na kumtegemea na kumtanguliza Mungu katika kila kitu, kila hatua.

“Pia, kuwa na nidhamu ya hali ya juu, bidii kwenye kila kitu ninachofanya kiwe kidogo au kikubwa, nafanya kwa bidii kubwa na maarifa makubwa, kuwa muadilifu, muaminifu, kuonesha na kusimamia ubora katika kazi ninayofanya na zaidi ni uamuzi wa kuendelea kujifunza kila siku,” alibainisha Zaipuna.

Aliupongeza uongozi wa Charlotte Sekondari na Bodi ya Shule chini ya Mwenyekiti Vidda-Joyce Makundi kwa kusimamia vema na kufanikisha elimu kwa wahitimu hao, huku akiwapongeza wazazi na walezi, akisema anaamini kuwa nyuma ya kila mtoto mdogo anayejiamini, kuna mzazi anayempa kujiamini huko.

Zaipuna alitumia nafasi hiyo kuwakumbusha wazazi na wanafunzi umuhimu wa kujenga utamaduni chanya wa kujiwekea akiba na kuwataka kujiunga na Jukwaa la Vijana la NMB liitwalo Go na NMB linalojumuisha elimu ya fedha, uwekaji akiba na suluhisho nyinginezo zikiwemo za bima ya afya.

Awali, Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Charlotte, Sista Monica Masaure, aliwashukuru wazazi kwa ushirikiano wao katika kujenga elimu ya watoto wao tangu mwaka 2021 walipojiunga, huku akiwapongeza walimu na wafanyakazi wasiokuwa waalimu kwa kusaidia ustawi wa taaluma shuleni kwake.

Sista Monica alibainisha kuwa dhamira yao kama shule ni kufuta ufaulu wa madaraja ya pili na tatu na kubaki na ‘Division One’ tu, msukumo unaopewa nguvu sio tu na ufundishaji wa walimu, bali misingi bora na imara iliyowekwa na wadau wa elimu wa shule hiyo ikiwemo Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.

Wakati wa Misa Takatifu kabla ya mahafali hayo, Padre Isdory Ndekumanya wa Shirika la Mapdre wa Maisha ya Kitume wa Kazi ya Roho Mtakatifu, aliwakumbusha wazazi na walezi wa wanafunzi wa Sekondari ya Charlotte kuwa msingi wa ‘Division One’ ya Elimu na Maisha kwa mtoto huwekwa tangu akiwa tumboni.

“Uzuri wa shule hupimwa kwa ufaulu katik eneo la taaluma, shule yenye ‘division one’ yenye pointi za juu, hii ndio shule bora, na ndio lengo na msukumo wa Charlotte Sekondari, ila kwa bahati mbaya shule nyingi zinasahau umuhimu wa malezi ya kiutu kwa watoto hawa, ambayo huanzia tumboni mwa mama.

“Hata kama tungeelimika namna gani, tukapata ‘degree’ na PhD za kutosha, kama tukikosa utu wema ni kazi bure, kwani tunaweza kuishi vema na kuyamudu mazingira ya maisha, lakini kuishi vema katika jamii ni kuwa na kujali utu.

“Kijana mwenye utu wema ni kijana msikivu, na kijana msikivu mara zote atakuwa na ufaulu wa masomo ya maisha na shuleni,” alibainisha Padre Ndekumanya wakati wa Misa Takatifu kuelekea sherehe za mahafali hayo ya wanafunzi 99.

Leave a Reply