Shirika la Changamoto za Milenia (Millennium Challenge Corporation-MCC) la Serikali ya Marekani limeeleza kuridhishwa kwake na mageuzi ya mifumo ya kiutendaji, yaliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita katika maeneo mbalimbali ikiwemo uimarishwaji wa demokrasia, utawala bora na haki za binadamu.
Hayo yamebainishwa wakati wa mkutano uliofanyika kati ya ujumbe wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ujumbe wa Shirika la Changamoto za Milenia uliofanyika terehe 17 Oktoba 2024 jijini Dodoma.
Akizungumza kwenye mkutano huo, Dan Barnes, Mkurugenzi wa Sera na Tathmini wa shirika hilo ambaye pia ameongoza ujumbe wa Marekani kwenye mkutano huo, ameeleza kuwa katika kipindi cha miaka mitatu ya Serikali hii, wameridhishwa na hatua mbalimbali zilizochukuliwa na Tanzania ambazo zimechangia kuongeza kasi ya maendeleo ya kiuchumi nchini.
Kadhalika, katika mkutano huo, Barnes alieleza kuwa Bunge la Marekani nalo limeridhia Tanzania kuendelea kunufaika na ufadhili wa Shirika hilo la MCC, baada ya kuridhishwa na utendaji wa Serikali ya Tanzania.
Maamuzi hayo yataifaya Tanzania kuendelea kupewa misaada katika shughuli za maendeleo ambazo zitasaidia kuinua uchumi wa mwananchi mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.
Hatua hii iliyofikiwa na MCC inatokana na dhamira ya dhati ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kufanya mageuzi na maboresho katika utendaji wake. Pamoja na sera madhubuti na uongozi thabit wa Serikali, mageuzi hayo yamefikiwa kupitia falsafa ya _4Rs_ ya Dk. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya maridhiano, ustahimilivu, mageuzi na ujenzi mpya iliyoleta mshikamano wa kisiasa, kijamii na kiuchumi nchini Tanzania. Falsafa hii imesaidia kuwavutia washirika mbalimbali wa maendeleo kote duniani wakiwemo MCC kwa manufaa ya pande zote.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mahamoud Thabit Kombo ameshiriki mkutano huo ambao ulijumuisha Mawaziri wanaosimamia sekta mbalimbali kutoka Tanzania Bara na Zanzibar zinazohusika moja kwa moja katika usimamizi na utekelezaji wa miradi mbalimbali inayofadhiliwa na MCC.
Akichangia katika mkutano huo Waziri Kombo ameeleza kuwa, Tanzania itaendelea kuheshimu na kuenzi uhusiano mzuri uliopo kati yake na Marekani uliodumu kwa zaidi ya miongo sita, huku zikishirikiana katika sekta mbalimbali ikiwemo elimu, afya, biashara na uwekezaji, kilimo, nishati, utalii, Teknolojia, ulinzi na madini. Sekta hizo zinafadhiliwa kupitia programu mbalimbali ikiwemo USAID, PEPFAR na Peace Corps.
Aidha, Waziri Kombo alisisitiza kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itaendelea kuheshimu na kutekeleza misingi ya demokrasia na utawala bora na haki za binadamu ambazo ni tunu za Tanzania na Marekani.
Uhusiano huo mzuri wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Marekani umeendelea kujidhihirisha kupitia ziara za viongozi Wakuu wa nchi ambapo mwaka 2023 Makamu wa Rais wa Marekani na Mgombea wa Urais wa Nchi hiyo kupitia chama cha Democrat Mhe. Kamala Harris alizuru nchini Tanzania.
Tanzania imekuwa ikinufaika na ufadhili wa miradi ya maendeleo kutoka MCC tangu mwaka 2005. Miradi hiyo ni pamoja na: ujenzi wa barabara ya Tunduma hadi Sumbawanga, Barabara za vijijini Pemba, barabara ya Tanga had Horohoro na barabara za ushoroba wa Mtwara.
Miradi mingine ni pamoja na; uwanja wa ndege wa Mafia, kuongezea uwezo mtambo wa kusukuma maji wa Ruvu chini na mradi wa kusambaza maji mjini Morogoro, maboresho na upanuzi wa njia za usambazaji wa nishati, mradi wa nishati ya jua mkoani Kigoma na miradi ya kujenga uwezo wa Shirika la Umeme la Tanzania (TANESCO) na Shirika la Umeme la Zanzibar (ZECO).
Shirika la Changamoto za Milenia ni taasisi ya Serikali ya Marekani iliyojikita katika kupunguza umasikini duniani kupitia programu mbalimbali zinazolenga kusaidia ukuaji wa uchumi, kwa kutoa ruzuku na misaada kwa nchi zinazokidhi viwango na vigezo thabiti vya utawala bora, mapambano dhidi ya rushwa, kuheshimu haki za binadamu na misingi ya kidemokrasia.