JUMLA ya Sh milioni 84 zinatarajiwa kutekeleza miradi ya ujenzi wa zahanati mbili, shule ya msingi na sekondari wilayani Magu, ikiwa ni mwendelezo jitihada serikali kuimarisha sekta ya elimu na afya nchini.
Akizungumza baada ya kumalizika kwa kikao cha kamati ya mfuko wa jimbo leo Jumanne wilayani Magu, Mwenyekiti wa kamati hiyo ambaye pia ni Mbunge wa Magu, Boniventura Kiswaga amesema kamati hiyo ilianza kujadili miradi iliyopatiwa fedha kwa mwaka 2024/2025 na kujiridhisha kuwa miradi hiyo imekamilika na kupongeza jitihada za wananchi kwa kuchangia kwa kiasi kikubwa nguvu kazi yao.
Aidha, Kiswaga amesema kamati imeridhia kutoa milioni 15 zinazoelekezwa kukamilisha ujenzi wa zahanati ya Nkunguru iliyopo Kata ya Nkunguru kwa asilimia 85, milioni 15 nyingine zimeelekezwa katika zahanati ya Kijiji cha Mwatelesha ili nayo ujenzi wake ufikie asilimia 85.

Kwa upande wa sekta ya elimu, Kiswaga amesema wamepeleka milioni 24 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa madarasa mawili ya shule ya Sekondari Simakitongo ambayo yalianza kujengwa kwa nguvu za wananchi hadi kufikia kwenye lenta.
“Tumepeleka milioni 30 kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya ya msingi Lugeye kwa sababu shule mama ya Salisima ina watoto zaidi ya 1,800 hivyo shule hii inatakiwa kugawanywa.
“Tunaishukuru halmashauri ilijenga madarasa mawili ambayo yapo asilimia 95 kwa hiyo wananchi wamejipanga kuanzisha maboma, hivyo tumepeleka milioni 30 ili kukamilisha madarasa mawili na watoto waanze kusoma hapo ili kupunguzia mzigo shule ya msingi Salisima,” amesema.
Kiswaga ametoa wito kwa wananchi wa Jimbo la Magu hasa sehemu ambazo kamati imeridhia kupeleka fedha za Mfuko wa Jimbo ili kuchochea Maendeleo wajitokeze kwa wingi kushirikiana na serikali ili kuhakikisha miradi hiyo inakamilika.
