You are currently viewing Mjane Alice akabidhiwa hati miliki ya nyumba na milioni 10

Mjane Alice akabidhiwa hati miliki ya nyumba na milioni 10

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amemkabidhi mjane Bi. Alice Haule hati miliki ya nyumba aliyoachiwa na marehemu mume wake huku akimchangia kiasi cha Shilingi Milioni 10 kwa ajili ya kuanzia maisha ikiwa ni dhamira ya ofisi ya Mkuu wa Mkoa ya kuendelea kuwasaidia wananchi wanaokabiliwa na changamoto mbalimbali za kijamii hususan wajane na yatima.

Hayo yamejiri wakati Serikali kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ikiwasilisha rasmi taarifa ya uchunguzi kuhusu mgogoro wa umiliki wa kiwanja namba 189 kilichopo eneo la Msasani Beach, baina ya mjane Alice Haule na Mohamed Yusufali jijini Dar es Salaam, kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila.

Akizungumza leo Oktoba 20, 2025, RC Chalamila amempa siku tano Mohamed Mustafa kujisalimisha kwenye ofisi ya Mkuu wa Mkoa kabla ya hatua zaidi hazijachukuliwa kuhusiana na sakata la nyumba lililomhusisha na mjane Bi. Alice Haule.

RC Chalamila amebainisha kuwa Bwana Mustafa amekuwa na maelezo yasiyoeleweka katika maelezo yake huku akiviagiza vyombo vya Dola kuendelea kumtafuta Mohamed kwa kutumia majina ya Viongozi katika maelezo yake kwa kujinasibu kuwa amekuwa na urafiki wa karibu na Viongozi.

Aidha, akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Dar es Salaam, Shukurani Kyando, amesema uchunguzi huo umefanyika kufuatia maagizo ya Mkuu wa Mkoa yaliyotolewa wiki mbili zilizopita, ambapo timu maalum iliundwa kupitia nyaraka, kuhoji wahusika na kuchambua mwenendo mzima wa umiliki wa kiwanja hicho.

Kamati pia imebaini kuwa mikataba ya mkopo na mauziano kati ya marehemu Lugaibula na Yusufali haikuwahi kuwasilishwa rasmi wizarani kama taratibu zinavyotaka.

Aidha, shahidi aliyekuwa wakili wa miamala hiyo alikiri mbele ya kamati kuwa marehemu Lugaibula ndiye aliyekuwa anaratibu mchakato wa kupata saini ya mkewe, Alice ingawa baadaye hakurejesha nyaraka hizo kwa ajili ya uthibitisho.

Akizungumza mara baada ya kupokea hati hiyo, Bi. Alice Haule amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwajali wanyonge pamoja na Mkuu wa Mkoa na vyombo vya habari kwa kushirikiana katika kupata haki yake.

Leave a Reply