You are currently viewing Museveni aongoza kwa asilimia 61.7 ya kura

Museveni aongoza kwa asilimia 61.7 ya kura

Matokeo ya awali yaliyotangazwa na tume ya uchaguzi ya Uganda yanampa ushindi Rais Yoweri Museveni kwa asilimia 61.7 ya kura halali ambazo zimekwisha hesabiwa hadi sasa.

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi nchini humo, Simon Mugenyi Byabakama ameyatoa matokeo hayo ya awali kwenye vyombo vya habari, matokeo ambayo yanaelekea kuendeleza utawala wa miongo minne wa Museveni.

“Yoweri Tibuhaburwa Kaguta Museveni wa chama cha NRM, amepata kufikia sasa kura 14,232, ambazo ni sawa na asilimia 61.7 ya kura halali zilizopigwa hadi sasa. Jumla ya kura halali kwa wagombea wote hadi sasa ni 23,049. Kura batili hadi sasa ni 796, ambazo ni sawa na asilimia 3.34 ya kura zote zilizopigwa, ” alitangaza Byabakama.

Matokeo rasmi ya uchaguzi huu huko Uganda yanatarajiwa kutolewa ndani ya saa 48 baada ya zoezi la upigaji kura kukamilika.

Katika baadhi ya maeneo, maafisa wa uchaguzi walionekana wakihesabu kura kwa uwazi kabisa. Katika uwanja wa mpira mjini Kampala kwenye ngome ya upinzani, umati wa watu ulishangilia lilipotajwa jina la mgombea urais mwimbaji aliyegeuka kuwa mwanasiasa Robert Kyagulani maarufu  Bobi Wine .

Bobi Wine anaishutumu serikali kwa “wizi wa kura” na kuwakamata baadhi ya maafisa wa chama chake. Wine alisema baada ya kupiga kura kuwa uchaguzi unafanyika gizani ili kurahisisha udanganyifu unaokusudiwa wa utawala huku akiwahimiza watu wa Uganda kutokata tamaa.

Mwanasiasa mwingine mkuu wa upinzani, Kizza Besigye, ambaye alichuana mara nne dhidi ya Museveni, alitekwa nyara nchini Kenya mwaka 2024 na kufikishwa katika mahakama ya kijeshi ya Uganda na sasa anakabiliwa na kesi ya uhaini inayoendelea. Vituo vya kupigia kura vilifungwa Alhamisi jioni kote nchini Uganda baada ya uchaguzi kufanyika licha ya kasoro mbalimbali kushuhudiwa, ikiwa ni pamoja na matatizo ya kiufundi, vituo kuchelewa kufunguliwa, masunduku ya kura kutowasili kwa wakati, kuzimwa kwa mtandao wa intaneti ambapo ulisababisha pia mitambo ya upigaji kura kwa njia ya kielektroniki kushindwa kufanya kazi ipasavyo.

Rais wa sasa wa Uganda Yoweri Museveni, mwenye umri wa miaka 81 ambaye aliingia madarakani mwaka 1986, anatarajiwa kushinda muhula wa saba kutokana na udhibiti wake kamili kwenye serikali pamoja na vyombo vya usalama.

 Museveni mwenyewe amekiri kuwepo na shida kwenye mashine za kupigia kura na akaahidi kuwa uchunguzi utafanyika.

Msemaji wa Shirika la Msalaba Mwekundu la Uganda, ambalo liliwatuma maafisa wake kote nchini humo kabla ya uchaguzi, ameliambia shirika la habari la AFP kwamba hawakupata ripoti zozote za vurugu licha ya uwepo mkubwa wa maafisa wa polisi na jeshi ili kuzuia uwezekano wa maandamano yenye vurugu kama ilivyoshuhudiwa katika mataifa jirani ya Kenya na Tanzania.

Waganda wengi bado wanamsifu rais  Yoweri Museveni  kama mtu aliyemaliza vurugu za baada ya uhuru na kusimamia ukuaji wa haraka wa uchumi, lakini baadhi ikiwemo idadi kubwa ya vijana wanamlaumu kutokana na mfululizo wa kashfa kubwa za ufisadi na wana matumaini ya kuwepo mabadiliko ya uongozi.

Leave a Reply