Takriban watu 130 wameokolewa baada ya meli ya kitalii iliyokuwa imetia nanga katika jiji la New Orleans, nchini Marekani, kugongwa na meli ya kubeba mizigo na kusababisha kupinduka na kulala ubavu ndani ya Mto Mississippi.
Meli hiyo ya kitalii iliyofahamika kwa jina la American Heritage, iligongwa na meli ya mizigo iitwayo Atlantic Asphalt, na kusababisha kuanza kuingia maji kabla ya kupinduka na kulala ubavu ndani ya mto huo.
Taarifa zinaeleza kuwa watu 32 waliokuwa ndani ya meli hiyo walikimbizwa hospitalini kwa ajili ya matibabu baada ya kupata majeraha yasiyo ya hatari kwa maisha yao. Hata hivyo, mamlaka zimethibitisha kuwa hakuna mtu aliyepotea au ambaye hajulikani alipo kufuatia ajali hiyo.

Tukio hilo limeelezwa kuwa la kimiujiza katika Mto Mississippi (Miracle on the Mississippi), kutokana na idadi kubwa ya watu waliookolewa bila kupoteza maisha.
Meya wa jiji la New Orleans, Helena Moreno, amesema mafanikio ya zoezi la uokoaji yanapaswa kupongezwa kwa dhati kwa vikosi vya uokoaji na wananchi walioshiriki katika kuwasaidia abiria waliokuwa hatarini.
“Tuna watu sifuri ambao hawajulikani walipo. Kwa kweli, huu ni muujiza katika Mto Mississippi,” alisema Moreno wakati akizungumza na waandishi wa habari.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Mamlaka ya Bandari ya New Orleans, Melanie Montroll, taarifa za ajali hiyo zilianza kupokelewa majira ya saa 1:30 alasiri kwa saa za Marekani siku ya Ijumaa, huku watu mbalimbali wakianza kutoa msaada kwa abiria waliokuwa wakijaribu kujinusuru wakati maji yakiingia ndani ya meli.
Wakati ajali inatokea, meli hiyo ilikuwa na takriban abiria 129 pamoja na wahudumu wake. Abiria walianza kushuka baada ya meli kuanza kuinamia upande mmoja kabla ya hatimaye kupinduka.
Waendeshaji wa boti za kuvuta meli, polisi na vikosi vingine vya uokoaji waliwasili haraka eneo la tukio kutoa msaada. Wakati wa operesheni hiyo, mamlaka zilisimamisha kwa muda shughuli za usafiri wa majini katika sehemu ya Mto Mississippi ili kurahisisha zoezi la uokoaji.
Akizungumzia chanzo cha ajali hiyo, Kamanda wa Jeshi la Walinzi wa Pwani la Marekani, Melanie Burnham, amesema uchunguzi bado unaendelea, lakini dalili za awali zinaonesha huenda meli hiyo ilipoteza uwezo wa kuongozwa au kudhibiti mwelekeo wake.
Rais wa Marekani, Donald Trump, kupitia mtandao wake wa Truth Social, amepongeza juhudi za uokoaji na kuzielezea kuwa ni kazi ya kipekee na ya kuvutia.
Meli ya American Heritage, inayoendeshwa na kampuni ya American Cruise Lines, ilikuwa inakamilisha safari ya kitalii ya siku nane iliyohusisha maeneo mbalimbali katika majimbo ya Louisiana na Mississippi.
Kwa mujibu wa taarifa zilizochapishwa kwenye tovuti ya kampuni hiyo, meli hiyo iliyojengwa mwaka 2015 ina uwezo wa kubeba hadi wageni 150.
