Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma ametoa maagizo kwa Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBRC) kuweka vigezo vya mabondia kuingia kwenye ngumi za kulipwa.
Maagizo hayo ameyatoa leo tarehe 11 Januari 2025 jijini Dar es salaam alipokutana na mapromota wa ngumi za kulipwa kwa ajili ya kujadili mambo mbalimbali yanayohusiana na mchezo huo.
“TPBRC mnatakiwa kuweka vigezo vya muda wa bondia kucheza ngumi za kulipwa, awe amecheza ngumi za ridhaa, kwa muda gani au mapambano mangapi anatakiwa kucheza ili aweze kuingia katika kigezo hicho”
“Hivi sasa mabondia wengi wanaingia moja kwa moja kulipwa bila kupitia ngumi za ridhaa, TPBRC nahitaji kupata majibu Januari 15, 2025, mapambano mangapi wanatakiwa kupitia,” amesema Mwinjuma.
Katika hatua nyingine amelitaka Bazara la Michezo la Taifa (BMT) kuwasaidia Mabondia na wanamichezo kufuta utaratibu wa kuomba vibali vya safari mapema, badala kuomba vibali kwa kuchelewa.
“Vibali vyote vya kusafiri vifuate utaratibu, mtu akienda uwanja wa ndege halafu anapiga simu au bado siku chache kwenda safari kwa ajili ya pambano, hakuna kutoa, huruma hiyo ife,” amesema Mwinjuma