You are currently viewing Nahodha wa MV Mwanza asimamishwa kazi

Nahodha wa MV Mwanza asimamishwa kazi

Waziri  wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, ameiagiza Kampuni ya Huduma za Meli (TASHICO) kumsimamisha kazi nahodha wa meli mpya ya kisasa ya New MV Mwanza, Adam Mwisungu, kufuatia ajali iliyotokea Novemba 18, mwaka huu baada ya meli hiyo kugonga mwamba wa Bismarck jijini Mwanza katika Ziwa Victoria.

Hatua hiyo imekuja baada ya uchunguzi wa ajali hiyo kubaini kuwa chanzo chake ni makosa ya kibinadamu na si hitilafu ya kiufundi, kama ilivyodaiwa katika baadhi ya taarifa zilizokuwa zikisambaa.

Akizungumza leo jijini Mwanza wakati akitoa taarifa ya uchunguzi, Profesa Mbarawa amesema uchambuzi wa mazingira ya tukio, mahojiano na wahusika pamoja na ukaguzi wa mifumo ya chumba cha injini, ulithibitisha kuwa mifumo yote ya meli ilikuwa ikifanya kazi vizuri.

Amekanusha pia taarifa zilizodai kuwa propela ya meli hiyo ilipinda baada ya kugonga jiwe katika eneo la mwamba wa Bismarck wakati wa majaribio ya kawaida.

Amesema teknolojia ya New MV Mwanza inahitaji wahudumu wenye uzoefu, umahiri na uwezo wa kufanya maamuzi ya haraka wanapokabiliwa na mazingira ya dharura.