Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Ng’wasi Kamani ameipongeza halmashauri ya wilaya ya Magu kwa kuweka mazingira bora yanayovutia wawekezaji mbalimbali hususani katika sekta ya ufugaji wa samaki hali inayochangia kuongeza ajira kwa vijana wazawa pamoja na kujifunza teknolojia za kisasa za ufugaji wa samaki aina ya sato.
Pia ameiagiza halmashauri hiyo kuendelea kuboresha ushirikiano na wawekezaji hao ili waendelee kuvuta wengina kuja kuwekeza nchini na kukuza sekta ya mifugo na uvuvi nchini.
Naibu Waziri huyo ametoa kauli hiyo jana Septemba 14, 2026, wilayani Magu mkoani Mwanza, wakati wa ziara maalum ya kikazi ya kuwatembelea wawekezaji katika tasnia ya ukuzaji viumbemaji, ikiwemo Tangreen Farming Company na M/S ROFI Farming Company Limited, kwa lengo la kujionea shughuli za uzalishaji zinazofanyika katika sekta hiyo.
Tangreen Farming Company ni kampuni kilichopo katika Kata ya Nyanguge kikiwa kinajishughulisha na uzalishaji samaki kwa njia ya vizimba ilihali kampuni ya M/S ROFI Farming Company Limited iliyopo kata ya Chabula, nayo inazalisha samaki kwa njia ya vizimba pamoja na chakula cha Samaki.
Pamoja na mambo mengine amewataka wawekezaji hao wa kuendelea kuwekeza katika sekta ya mifugo na uvuvi, huku wakizingatia ustawi na usalama wa wafanyakazi wao pamoja na kuhakikisha wanazalisha kwa tija.
Aidha, Kamani amewataka wananchi kutumia fursa zinazotokana na uwekezaji kwa kujifunza ujuzi na teknolojia kutoka kwa wawekezaji, hatua ambayo itawawezesha kuongeza uzalishaji na kujiajiri katika shughuli za mifugo na uvuvi.
Katika hatua nyingine, amewataka wataalam wa serikali kuongeza jitihada za kutatua changamoto ya upatikanaji wa chakula cha samaki na mifugo, ikiwemo kuongeza uzalishaji wa chakula hicho kwa wingi na kwa gharama nafuu, ili kuwawezesha wafugaji na wafugaji wa samaki kuongeza uzalishaji.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmshauri ya Wilaya, Mohamed Ramadhani alisema wawekezaji hao wameleta manufaa mengi ndani ya wilaya ikiwamo kuchangia uwepo wa uhakika wa ajira kwani hadi sasa zaidi ya asilimia 80 ya wafanyakazi wa kampuni hizo ni wananchiwa wilaya ya Magu.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Mhandisi Edward Kihamba alisema wawekezaji hao wamesaidia kukuza bajeti ya halmashauri kutoka sh bilioni 4.2 mwaka 2024/2025 hadi kufikia Sh bilioni sita.
Wakati mkuu wa wilaya ya Magu, Jubilate Lawuo alisisitiza kuwa wataendelea kuweka mazingiza mazuri kwa wawekezaji ikiwamo kutekeleza maagizo yote yanayotolewa na mamlaka husika katika sekta hiyo ya uvuvi.
