You are currently viewing NCAA yajinoa kushiriki michuano ya SHIMMUTA 2024 Tanga

NCAA yajinoa kushiriki michuano ya SHIMMUTA 2024 Tanga

Na Mwandishi Wetu, Tanga

Timu ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) imewasili mkoani Tanga kushiriki kikamilifu katika Mashindano ya Mashirika ya Umma, Makampuni na Taasisi Binafsi (SHIMMUTA) yanayoanza leo tarehe 10 hadi 24 Novemba 2024, jijini Tanga. 

Mashindano haya yanajumuisha mashirika mbalimbali nchini yakiwa na lengo la kukuza mshikamano, afya, na ari ya ushindani miongoni mwa wafanyakazi wa mashirika hayo.

Nelson Mshanga, mmoja wa wachezaji mahiri wa timu ya kamba ya NCAA, ameshukuru uongozi wa mamlaka kwa kuwapa msaada na motisha inayowawezesha kushiriki mashindano haya kwa nguvu na hamasa kubwa huku wakiwa na ari mpya ya ushindi.

Nelson alieleza kuwa timu yao ipo na nguvu mpya kutokana na kuongezeka kwa vijana walioajiriwa hivi karibuni, ambao wameleta mtazamo, nguvu na ari mpya ya ushindi.

“Tumekuwa na maandalizi bora zaidi kuliko mwaka jana. Uongozi umetupa kila tunachohitaji ili tuweze kuwakilisha NCAA kwa heshima na nguvu,” alisema Nelson.

Kapteni wa timu ya mpira wa pete ya NCAA, Halima Mbombe, ametoa hakikisho kwa mashabiki na wapenzi wa timu ya Ngorongoro kuwa, wamejipanga kurudi nyumbani wakiwa na vikombe.  

Halima amesema “Tumekuwa na ratiba maalum ya mazoezi na nidhamu ya hali ya juu, mashabiki wetu watarajie mafanikio makubwa. Ushindi ni lazima,” alisema kwa kujiamini.

Hamis Mshana, mkufunzi wa timu ya mpira wa miguu ya NCAA, amesisitiza dhamira yao ya kurudi nyumbani na vikombe zaidi. Hamis ameweka wazi kuwa timu imekuwa ikifanya mazoezi makali na yenye malengo ya kupata ushindi wa hali ya juu. Kwa msaada wa vifaa vya kisasa na ushirikiano wa uongozi, timu ya mpira wa miguu inategemea kufanya vizuri na kuwafurahisha mashabiki wao.

Kushiriki kwa NCAA kwenye SHIMMUTA 2024 sio tu kunaleta ushindani, bali pia kunajenga mshikamano wa ndani na kuimarisha afya za wafanyakazi. 

Mashindano haya yanatoa fursa kwa wafanyakazi wa NCAA kushiriki michezo mbalimbali kama vile mpira wa miguu, mpira wa pete, mpira wa kikapu, mpira wa wavu, riadha, kamba na mingineyo ambapo michezo hii inaenda sambamba na kuhamasisha utalii wa ndani kwa vivutio vya utalii vilivyopo Ngorongoro.

Leave a Reply