BENKI ya NMB kwa kushirikiana na Mamlaka ya udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) imezindua huduma ya uhakiki wa dhamana za zabuni za kibenki kupitia mfumo wa NeST.
NeST ni mfumo wa kielektroniki ambao sasa umeunganishwa rasmi na mifumo ya NMB kwa lengo la kuboresha mfumo wa ununuzi wa umma na kuwawezesha wafanyabiashara kushindana kwa uwazi na haki.

Mkurugenzi Mtendaji wa NMB, Bi. Ruth Zaipuna pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa PPRA, Dennis Simba wamezindua mfumo huo leo Alhamisi jijini Dar es Salaam na kubainisha kuwa huduma zitaanza kutolewa rasmi kwa wazabuni wote wanaotumia mfumo wa NeST kuanzia mwezi huu.
Akifafanua kuhusu huduma hizo, Simba amesema kupitia mfumo huu, benki inaweza kutoa dhamana kwa kuhakiki na kumpatia mzabuni namba ya dhamana.
“Namba hiyo ikiingizwa kwenye mfumo wa NeST, uthibitisho wake hufanyika papo hapo, bila taasisi nunuzi kuwasiliana na benki kwa njia za kawaida kwa lengo la kuthibisha.
“Mfumo unathibitisha uhalali wa dhamana, thamani yake, muda wake wa uhai, na uhusiano wake na zabuni husika. Hatua hii itapunguza muda wa zabuni, kuongeza uwazi, na kuimarisha imani katika mfumo wa ununuzi wa umma,” amesema na kuongeza;
“Shukurani pia kwa Benki ya NMB kwa kuhakikisha inaungana katika kuhakikisha maelekezo ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa “mifumo isomane”, yanatimia na kuwasaidia wazabuni ambao ni wateja wao kukamilisha michakato ya kuomba zabuni kwa urahisi zaidi na haraka”.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa NMB, Bi. Ruth Zaipuna amesema mfumo huo unalenga kurahisisha mchakato, kuboresha ufanisi wa utendaji kazi kwa wataalamu wa ugavi na ununuzi.
Amesema hatua hiyo inaonesha sio tu ubunifu na maendeleo ya taasisi, bali pia dhamira ya NMB kutumia teknolojia za kisasa na ushirikiano wa kimkakati kubuni masuluhisho bora ya kifedha yanayozingatia muda, usalama, na uwazi.

“Lengo ni kuongeza ufanisi katika sekta mbalimbali – ikiwemo ununuzi wa umma – na kuchochea ukuaji endelevu wa uchumi wa taifa.
“Ubunifu huu unarahisisha mchakato wa dhamana za benki katika ununuzi wa umma, unapunguza muda wa kukamilisha taratibu, na unaimarisha uzingatiaji wa kanuni za ununuzi. Vilevile, unachangia kuongeza uwazi na kuimarisha uhusiano kati ya taasisi za serikali na wadau wa zabuni,” amesema.
Amesema kwa kushirikiana na PPRA, NMB inalenga kuhakikisha wateja na wadau wanapata huduma rahisi, ya kuaminika, na yenye uhakika zaidi.
Amesema kupitia muunganiko huo wa kidijitali wa mifumo ya NMB, benki hiyi inaendelea kuthibitisha nafasi yake kama mshirika mkuu wa kifedha katika kuendeleza mageuzi ya kidijitali na kuboresha utoaji wa huduma nchini.
Kwa mujibu wa PPRA tangu michakato yote ya zabuni za Serikali kufanyika kupitia mfumo wa NeST, sasa mfumo huo unasomana na taasisi zaidi ya 20, zikiwemo taasisi za kibenki.
