Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Katika kuendelea kuwa mshirika mkubwa wa maendeleo nchini, Benki ya NMB imetunukiwa tuzo tatu na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), ikiwa ni sehemu ya juhudi za TRA kuthamini mchango wa walipa kodi katika maendeleo ya Taifa.
Tuzo hizo zinazoitambua Benki ya NMB kama mlipa Kodi Mkubwa Zaidi na Bora Zaidi nchini Tanzania kwa mwaka wa kifedha 2023/2024 ni: Mshindi wa Kwanza; Taasisi inayolipa kodi kubwa na inayozingatia misingi na kanuni bora za ulipaji kodi (sekta ya kibenki).

Pia Mshindi wa Kwanza; Mchangiaji bora wa ukusanyaji kodi nchini na Mshindi wa kwanza; Taasisi inayolipa kodi kubwa zaidi nchini na kuzingatia kanuni za ulipaji kodi (sekta zote nchini).
Tuzo hizi zimetolewa jana tarehe 23 Januari 2025 na Rais Samia Suluhu Hassan, kwenye Siku ya Shukrani na tuzo kwa Mlipa Kodi na kupokelewa kwa niaba ya Benki na Afisa Mtendaji Mkuu wetu, Ruth Zaipuna.
Zaipuna amesema mafanikio haya kwa benki ya NMB ni matokeo ya kuzingatia kanuni bora za ulipaji kodi, ufanisi katika kujiendesha na ubunifu wa suluhishi bora za kifedha zenye manufaa kwa Wateja na Taifa letu.
“Dhamira yetu ni kuendelea kuendesha biashara ya kutoa huduma za fedha kwa kuzingatia sheria na kanuni za nchi ili kuchangia kikamilifu ujenzi wa uchumi wa Tanzania,” amesema.