Rais wa Urusi, Vladimir Putin, amesema Urusi itaendelea kuimarisha ushirikiano wake na Tanzania kwa kuongeza fursa za kiuchumi na kidiplomasia kati ya nchi hizo mbili, akisisitiza kuwa uhusiano huo unaendelea kukua kwa kasi na una mustakabali mzuri zaidi.
Putin amesema hayo wakati ambao biashara kati ya Urusi na Tanzania imeongezeka kwa takribani asilimia 20 hadi 25 mwaka 2025, na kwamba bado kuna nafasi kubwa ya kupanua zaidi sekta ya biashara kupitia maeneo muhimu kama nishati, usafirishaji, afya, elimu na utafiti wa kisayansi.
Akizungumza wakati wa mazungumzo na Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Ikulu yw Kremlin, Putin amesema kuwa mwaka huu una umuhimu wa kihistoria kwa kuwa nchi hizo mbili zinasherehekea miaka 65 ya uhusiano wa kidiplomasia, akieleza pia furaha yake kuona Rais Samia akichagua Urusi kuwa nchi ya kwanza kufanya ziara ya kikazi baada ya uapisho wa uongozi wake kipindi cha pili.
Aidha, Putin amesisitiza kuwa ushirikiano kati ya nchi hizo umeendelea kuimarika katika sekta mbalimbali za maendeleo, hususan nishati, miundombinu ya usafirishaji, afya, elimu na utafiti, ambazo zinaweza kuongeza manufaa kwa pande zote mbili.
Katika hitimisho, amesema Urusi inaendelea kuona Tanzania kama mshirika muhimu wa kimkakati katika majukwaa ya kimataifa, na akatarajia ushirikiano zaidi kuimarika kupitia mikutano ijayo ikiwemo Jukwaa la Uchumi la St Petersburg na Mkutano wa Tatu wa Urusi na Afrika.
