Rais Samia Suluhu Hassan ameomboleza kifo cha Askofu Mkuu mstaafu wa jimbo kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo aliyefariki dunia usiku wa Februari 19, 2026.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Askofu mkuu wa jimbo kuu la Dar es Salaam, Yuda Thaddeus Ruwa’ich, Kardinali Pengo alifariki dunia saa 4:00 usiku wa Februari 19, 2026 alipokuwa akipatiwa matibabu katika taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) jijini Dar es Salam.
Aidha, katika salamu zake za rambirambi leo Februari 20, 2026 kupitia taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu, Rais Samia amesema amepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha Kardinali Pengo.
“Katika kipindi chote cha utumishi wake, Kardinali Pengo alisimama imara katika kuhubiri amani, maadili na mshikamano wa kitaifa.
“Alikuwa sauti ya busara katika masuala ya kijamii na kimaadili, akihimiza amani, heshima na utu katika jamii yetu. Mchango wake katika malezi ya kiroho na maendeleo utaendelea kukumbukwa na kuenziwa siku zote.
“Ninatoa pole kwa Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Askofu Wolfgang Pisa, Maaskofu, Mapadri, Watawa, familia, ndugu, jamaa, marafiki, waumini wa Kanisa Katoliki na Watanzania wote kwa msiba huu. Mwenyezi Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi,” amesema Rais Samia.
