Rais Samia Suluhu Hassan, amewataka viongozi wapya wa Tume za Haki za Binadamu na Utawala Bora, kufuatilia mwenendo wa haki binadamu wa ndani na nje ya nchi na kutoa majibu ya haraka kuhusu shutuma zinazoelekezwa Tanzania.
Dkt Samia ameeeleza hayo leo Jumatatu Novemba 2,2026 wakati akiwaapisha viongozi hao wateule, Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma.
“Nataka niwaambie katika dunia ya leo, mambo yapo juu chini.Mwenye haki, ataambiwa huna haki na asiyekuwa na haki, anaambiwa ana haki,” amesema na kuongeza kuwa;
“Hii Tume ya Haki na Utawala Bora, ili kuwa na utawala bora, lazima muone tunashutumiwa na nini nje, na hali ndani ikoje na mjibu kwa haraka,” amesema Dkt Samia.
Kwa mujibu wa Dkt Samia, mataifa yanayofanywa vizuri kwa sababu hazipendezi machoni kwa wengine, zitaambiwa hazina haki za binadamu na zile zinazovunjwa kwa sababu zina nguvu, zinaambiwa hazivunji haki.
“Nawaombeni sana nyie ni vijana, mna uwezo wa kuperuzi mitandao yote mkaona yanayotokea duniani, mkaona shutuma tunazopewa na mkazijibu,” amesisitiza Mkuu huyo wa nchi.
