Rais Samia Suluhu Hassan, amezindua rasmi ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR), kipande cha sita kutoka Tabora hadi Kigoma, yenye urefu wa kilomita 506.
Mradi huo, utagharimu Sh6.23 trilioni kwa kipande cha Tabora-Kigoma, kipande cha Uvinza-Msongati kikigharimu Sh3.17 trilioni na vyote ujenzi wake utakamilika mwaka 2030.
Rais Samia amezindua ujenzi huo leo, Julai 20, mkoani Kigoma kwa kuweka jiwe la msingi.
Mradi huo pia, unatarajiwa kupunguza muda wa safari kutoka Dar es Salaam kwenda Kigoma kutoka zaidi ya saa 20 za sasa hadi saa nane, huku ukanda wa Magharibi ukitarajiwa kufunguliwa kiuchumi.
Kadhalika, ujenzi huo ambao kwa sasa umefikia zaidi ya asilimia 10, utazalisha ajira 15,000 kwa wananchi wa Kigoma na Tabora, pia utaifungua Kigoma, Bandari ya Dar es Salaam na nchi jirani za Jamhuri ya Demokrasia ya Congo na Burundi.
