Rais Samia Suluhu Hassan amesema vurugu za Oktoba 29, zilipangwa, kugharimiwa na kuratibiwa na watu kutoka nje wakishirikiana na wa ndani, kwa lengo la kupindua nchi.
“Lile lilikuwa ni jambo la kupangwa na vurugu zile zilidhamiria makubwa. Vurugu zile ni mradi wenye nia ovu wenye wafadhili, washitiri na watekelezaji,” amesema.
Amesema vurugu hizo zilizoratibiwa na watu kutoka ndani na nje ya nchi, kati yao wapo wanaojulikana na wasiojulikana, hivyo Serikali inawatafuta ili kuwajua.
Ametaja baadhi ya sababu za kutaka kuipindua nchi, ni ushindani wa Tanzania kibiashara na utajiri mkubwa wa rasilimali, ikiwemo madini adimu.
Pamoja na hayo, Rais Samia amesema wapo walioingia kwa kufuata mkumbo kwa ahadi ya maisha mazuri baadaye.
Rais Samia ametoa kauli hiyo leo, Jumanne Desemba 2, 2025 katika hotuba yake kwa Taifa, wakati wa kikao chake na wazee wa Jiji la Dar es Salaam.
