Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Magu kwa kupata hati inayoridhisha ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa miaka minne mfululizo.
Amesema kutokana na uongozi bora, Halmashauri hiyo imekuwa ikizalisha hoja chache za ukaguzi, huku nyingi zikiwa zimejibiwa na nyingine zikiendelea kufanyiwa kazi.
Mtanda ametoa kauli hiyo leo Juni 25, 2026, alipokuwa akizungumza katika Mkutano Maalumu wa Baraza la Madiwani wa kujadili hoja za Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa Halmashauri ya Wilaya ya Magu.
Pamoja na mambo mengine amesisitiza ni muhimu Baraza la Madiwani kufahamu madeni yote ya wazabuni na watumishi ili kuweka mpango wa kuyapunguza hatua kwa hatua katika miaka ijayo.
“Watumishi wanaoidai halmashauri wanapaswa kubainishwa pamoja na madai yao ili kuwepo mpango maalumu wa kulipa madeni hayo kwa awamu na hivyo kupunguza mzigo wa kifedha,” amesema.
Aidha, amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Mohamed Ramadhan kuendelea kuimarisha ushirikiano na wataalamu wake bila ubaguzi.
Ametoa mfano kwamba MWEKA HAZINA anapaswa kutekeleza maagizo anayopewa na mkurugenzi bila kupendelea makundi ya watumishi walio karibu naye.
“Halmashauri inakusanya mapato ya ndani vizuri, kunapotokea maombi ya fedha, mkurugenzi ukapitisha, mweka hazina hapaswi kukataa kwa sababu kama hakuna fedha kutatokea makundi. Tusiendekeze kulambwa mikono… mkurugenzi akitoa maagizo watu wote watekeleze,” amesisitiza.
Kwa upande wake mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Magu, Mhandisi Edward Kihamba amesema ameyapokea maelekezo hayo na kuahidi kutekeleza huku akiwataka madiwani na wakuu wa idara kushirikiana kukamilisha miradi kama ilivyoelekezwa.
