Na Mwandishi wetu, Katavi
Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA) imeendelea kutoa mafunzo kwa Viongozi wa Serikali wakiwemo Wakuu wa Wilaya, Maafisa Tawala, Maafisa Tarafa, vitongoji pamoja na Wazee wa Kimila kutoka mikoa sita ili waweze kusimamia vizuri migogoro inayotokana na mirathi, ndoa na talaka katika maeneo hayo.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo kwa viongozi hao kutoka mikoa ya (6) ya Katavi, Kigoma, Tabora, Rukwa, Mbeya na Songwe katika mkutano wa siku mbili uliofanyika mikoa ya Katavi, Kabidhi Wasii Mkuu na Afisa Mtendaji Mkuu wa RITA Bw. Frank Kanyusi, amesisitiza umuhimu wa kuzingatia sheria katika masuala ya wosia, mirathi, ndoa na talaka ili kupunguza migogoro ya kifamilia na kulinda haki za warithi halali.

“Viongozi wa ngazi za msingi wana nafasi ya kipekee katika kutoa elimu kwa jamii na kusimamia utekelezaji wa sheria katika maeneo yao ya kazi na hivyo kupunguza migogoro katika jamii,” alisisitiza Bw. Kanyusi.
Bw. Kanyusi alisema kupitia mafunzo hayo, walipata fursa ya kujua taratibu za uandishi na uhifadhi wa wosia, usajili wa mirathi, pamoja na wajibu wa viongozi wa kimila katika kuhakikisha mgawanyo wa mali unafanyika kwa kuzingatia sheria za nchi.
Aidha, Bw. Kanyusi aliwataka viongozi hao licha ya kutumia sheria na taratibu zilizowekwa watumie pia busara kutatua changamoto zinazoikumba jamii kwani wao wapo karibu zaidi na wananchi.
Kwa upande wake Afisa Msajili Msaidizi Mkuu kutoka RITA, Bi. Victoria Mushi ambaye ni miongoni mwa wawezeshaji katika mafunzo hayo alielezea faida za mwananchi kuandika wosia mapema na kuhifadhi nyaraka hizo kwa mujibu wa utaratibu rasmi kwani kwa kufanya hivyo itaepusha migogoro isiyo ya lazima kwa warithi pindi mmiliki anapofariki.
“Tumeshuhudia jamii nyingi zikiingia katika migogoro mikubwa hasa ya mirathi na hiyo yote ni kutokana na ukosefu wa elimu ya kuandaa wosia hivyo,”
“Hivyo, kupitia muendelezo wa mafunzo haya tunauhakika yatasaidia kupunguza kwa kiasi kikubwa migogoro hiyo,” alisisitiza Bi. Mushi.
Naye Mkuu wa Wilaya ya mpanda.Bi. Jamila Yusuph, mbali ya kuipongeza RITA kwa kuandaa mafunzo hayo, amesisitiza umuhimu wa viongozi hao kutoa mwongozo kwa wananchi kuhusu huduma za RITA zinazopatikana kupitia mfumo wa eRITA, hasa kwa usajili wa ndoa, talaka, wosia na udhamini wa mirathi.
“Kupitia mafunzo haya yataongeza uwazi katika utoaji huduma sambamba na utoaji elimu katika jamii kwa kushirikiana na wadau mbalimbali katika ngazi zote za uongozi ili kulinda haki za wananchi pamoja na kupunguza migogoro,” alisema Bi. Yusuph.
Miongoni mwa Wazee wa Kimila, Bw Nelson Majura amesema kupitia mafunzo hayo, yamewajengea uwezo wa kutoa mwongozo sahihi kwa wananchi na kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na taasisi za kimila katika kusimamia masuala ya mirathi.
Mkutano huo ni sehemu ya mkakati wa RITA wa kuendelea kutoa elimu kwa umma na viongozi wa ngazi mbalimbali ili kuhakikisha haki, uwazi na utawala bora vinazingatiwa katika utoaji wa huduma kwa wananchi.
